1 Basi hawa watu watatu: Elifazi, Bildadi na Sofari, wakaacha kumjibu Yobu kwa vile alijiona kuwa mwema.
2 Ndipo Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa ukoo wa Rama, akakasirika. Alimkasirikia Yobu kwa sababu Yobu alijiona yeye mwadilifu na sio Mungu.
3 Pia, aliwakasirikia rafiki watatu wa Yobu kwa sababu hawakuwa na la kumjibu Yobu, na hivyo kuonesha kwamba Mungu amekosa.
4 Elihu alikuwa amekaa kimya wakati hao wazee waliposema na Yobu kwa kuwa yeye alikuwa kijana kuliko wao.
5 Lakini alipoona hao watu watatu wameshindwa kumjibu Yobu, aliwaka hasira.
6 Basi, Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi akaanza kusema:“Mimi ni kijana, nyinyi ni wazee zaidi;kwa hiyo niliogopa kuwaambieni mawazo yangu.
7 Nilisema moyoni: ‘Waache wenye siku nyingi waseme,wenye miaka mingi wafundishe hekima.’
8 Lakini hiyo roho iliyomo ndani ya mtu,hiyo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu,ndio inayomwezesha mwanadamu kufahamu.
9 Si lazima kuwa mzee ili uwe na hekimawala wazee siyo wenye kufahamu lililo sawa.
10 Kwa hiyo nasema, ‘Nisikilizeni,acheni nami nitoe maoni yangu.’
11 “Basi, mimi nilingojea mlichotaka kusema,nilisikiliza misemo yenu ya hekima,mlipokuwa mnajaribu kutafuta la kusema.
12 Niliwasikiliza kwa makini sana,lakini hakuna mmoja wenu aliyemshinda Yobu;nyote mlishindwa kuyajibu maneno yake.
13 Jihadharini msije mkasema, ‘Sasa tumepata hekima.Atakayemshinda ni Mungu, sio binadamu.’
14 Maneno ya Yobu hayakuwa kwa ajili yangu,kwa hiyo sitamjibu kama mlivyomjibu nyinyi.
15 “Nyinyi mmeduwaa; mmeshindwa,nyinyi hamna cha kusema zaidi.
16 Je, ningoje tu kwa vile hamsemi,kwa sababu mnakaa tu bila kujibu kitu?
17 Mimi pia nitatoa jibu langu;mimi nitatoa pia maoni yangu.
18 Ninayo maneno mengi sana,roho yangu yanisukuma kusema.
19 Moyo wangu umefurika kama divai iliyozibwa,kama kiriba cha divai mpya tayari kupasuka.
20 Ni lazima niseme ili nipate nafuu;yanipasa kufungua kinywa changu na kujibu.
21 Sitampendelea mtu yeyotewala kutumia maneno ya kubembeleza mtu.
22 Maana mimi sijui kubembeleza mtu,la sivyo, Muumba wangu angeniangamiza.