1 “Hakika kuna machimbo ya fedha,na mahali ambako dhahabu husafishwa.
2 Watu huchimba chuma ardhini,huyeyusha shaba kutoka mawe ya madini.
3 Wachimba migodi huleta taa gizani,huchunguza vina vya ardhina kuchimbua mawe yenye madini gizani.
4 Binadamu huchimba mashimo mbali na makazi ya watu,mbali na watu mahali kusipofikika,wachimba madini huninginia wamefungwa kamba.
5 Kutoka udongoni chakula hupatikana,lakini chini yake kila kitu huvurugwa kwa moto.
6 Katika mawe yake ndimo vilimo vito vya rangi ya samawatina udongo wake una vumbi la dhahabu.
7 “Njia za kwenda kwenye migodi hiyohakuna ndege mla nyama azijuaye;na wala jicho la tai halijaiona.
8 Wanyama waendao kwa madaha hawajazikanyagawala simba hawajawahi kuzipitia.
9 Binadamu huchimbua miamba migumu kabisa,huichimbua milima na kuiondolea mbali.
10 Hupasua mifereji kati ya majabali,na jicho lake huona vito vya thamani.
11 Huziba chemchemi zisitiririke,na kufichua vitu vilivyofichika.
12 “Lakini hekima itapatikana wapi?Ni mahali gani panapopatikana maarifa?
13 Hakuna mtu ajuaye thamani ya hekima,wala hekima haipatikani nchini mwa walio hai.
14 Vilindi vyasema, ‘Hekima haimo kwetu,’na bahari yasema, ‘Haiko kwangu.’
15 Hekima haiwezi kupatikana kwa dhahabu,wala kwa kupima kiasi kingi cha fedha.
16 Haiwezi kupimwa kwa dhahabu ya Ofiri,wala kwa vito vya Sardoniki au vya rangi ya samawati,
17 dhahabu au kioo havilingani nayo,wala haiwezi kubadilishwa na vito vya dhahabu safi.
18 Hekima ina thamani kuliko matumbawe na marijani,thamani yake yashinda thamani ya lulu.
19 Topazi ya Kushi haiwezi kulinganishwa nayo,wala haiwezi kupewa bei ya dhahabu safi.
20 “Basi, hekima yatoka wapi?Ni wapi panapopatikana maarifa?
21 Imefichika machoni pa viumbe vyote hai,na ndege wa angani hawawezi kuiona.
22 Abadoni na Kifo wasema,‘Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.’
23 “Mungu aijua njia ya hekima,anajua mahali inapopatikana.
24 Maana yeye huona mpaka upeo wa dunia,huona kila kitu chini ya mbingu.
25 Alipoupa upepo uzito wake,na kuyapimia maji mipaka yake;
26 alipoamua mvua inyeshe wapi,umeme na radi vipite wapi;
27 hapo ndipo alipoiona hekima na kuitangaza,aliisimika na kuichunguza.”
28 Kisha Mungu akamwambia mwanadamu:“Tazama! Kumcha Bwana ndio hekima;na kujitenga na uovu ndio maarifa.”