Yobu 22 BHN

Hoja ya Elifazi

1 Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu Yobu:

2 “Je, binadamu anafaa chochote kwa Mungu?Kwa kweli mwenye hekima anajifaidi mwenyewe tu.

3 Je, unadhani wamfurahisha Mungu kwa kuwa mnyofu?Au anapata faida gani kama huna hatia?

4 Unadhani anakurudi na kukuhukumukwa sababu wewe unamheshimu?

5 La! Uovu wako ni mkubwa mno!Ubaya wako hauna mwisho!

6 Wewe umemnyanganya ndugu yako nguo ya rehani;umemchukulia nguo hiyo moja aliyokuwa nayo.

7 Umewanyima maji wale waliokuwa wamechoka;umewanyima chakula wale walio na njaa.

8 Umemruhusu mwenye cheo kuchukua ardhi yote;umemwacha anayependelewa aishi humo.

9 Umewaacha wajane waende mikono mitupu;umewanyima yatima uwezo wao.

10 Kwa hiyo mitego imekuzunguka pande zote,hofu ya ghafla imekuvamia.

11 Giza limekuangukia usione kitu;mafuriko ya maji yamekufunika.

12 Twajua Mungu yuko huko juu mbinguni.Tazama nyota za juu kabisa zilivyo mbali!

13 Lakini wewe wasema: ‘Mungu ajua nini?Je, aweza kupenya mawingu akatoa hukumu?

14 Mawingu mazito yamemzunguka asipate kuonayeye hutembea nje ya anga la dunia!’

15 “Je, umeamua kufuata njia za zamaniambazo watu waovu wamezifuata?

16 Hao walifagiliwa kabla ya wakati wao,misingi yao ilikumbwa mbali na maji.

17 Hao ndio waliomwambia Mungu, ‘Achana nasi!’Na ‘Wewe Mungu Mwenye Nguvu waweza nini juu yetu?’

18 Lakini Mungu ndiye aliyejaza nyumba zao fanaka,lakini walimweka mbali na mipango yao!

19 Wanyofu huona na kufurahi,wasio na hatia huwacheka na kuwadharau,

20 Wanasema ama kweli maadui zetu wameangamizwa,na walichobakiza kimeteketezwa kwa moto.

21 “Sasa, Yobu, kubaliana na Mungu uwe na amani,na hapo mema yatakujia.

22 Pokea mafundisho kutoka kwake;na yaweke maneno yake moyoni mwako.

23 Ukimrudia Mungu na kunyenyekea,ukiondoa uovu mbali na makao yako,

24 ukitupilia mbali mali yako,ukaitupa dhahabu ya Ofiri ukingoni mwa kijito,

25 Mungu Mwenye Nguvu akawa ndio dhahabu yako,na fedha yako ya thamani;

26 basi, ndipo utakapomfurahia Mungu mwenye nguvuna kutazama kwa matumaini;

27 utamwomba naye atakusikiliza,nawe utazitimiza nadhiri zako.

28 Chochote utakachoamua kitafanikiwa,na mwanga utaziangazia njia zako.

29 Maana, Mungu huwaporomosha wenye majivuno,lakini huwaokoa wanyenyekevu.

30 Yeye humwokoa mtu asiye na hatia;wewe utaokolewa kwa matendo yako mema.”