1 Ndipo Bildadi, Mshuhi, akamjibu Yobu:
2 “Utasema mambo haya mpaka lini?Mpaka lini maneno yako yatakuwa matupu kama upepo?
3 Kwani, wadhani Mungu hupotosha haki?Au, je, Mungu Mwenye Nguvu hupotosha ukweli?
4 Kama watoto wako wamemkosea Mungu,yeye amewalipiza matokeo ya uhalifu wao.
5 Kama utamtafuta Munguukamsihi huyo Mungu mwenye nguvu,
6 kama wewe u safi moyoni na mnyofu,kweli Mungu atakuja kukusaidia,na kukujalia makao unayostahili.
7 Na ingawa ulianza kuishi kwa unyongemaisha yako ya baadaye yatakuwa ya fahari zaidi.
8 Jifunze tafadhali kwa wale waliotutangulia,zingatia mambo waliyogundua hao wazee.
9 Sisi ni watu wa juzijuzi tu, hatujui kitu;siku zetu duniani ni kivuli kipitacho.
10 Lakini wao watakufunza na kukuambia,mambo waliyopata kuyatoa katika maarifa yao:
11 Mafunjo huota tu penye majimaji,matete hustawi mahali palipo na maji.
12 Hata kama yamechanua na bila kukatwa,yakikosa maji hunyauka kabla ya mimea mingine.
13 Ndivyo walivyo wote wanaomsahau Mungu.Tumaini la wasiomwamini Mungu litapotea.
14 Tegemeo lao huvunjikavunjika,tumaini lao ni utando wa buibui.
15 Wanaegemea nyumba yao lakini haitasimama,huishikilia lakini haidumu.
16 Jua litokapo yeye hustawi;hueneza matawi yake bustanini mwake.
17 Mizizi yake hujisokotasokota kwenye mawenaye aenda kuchunguza ndani ya mwamba.
18 Lakini akiangamizwa kutoka makao yake,hayo yatamkana yakisema: ‘Sijapata kukuona.’
19 Tazama, huo ndio mwisho wa furaha ya mtu huyo,na mahali pao patachipua wengine.
20 “Tazama! Mungu hatamkataa mtu asiye na hatia,wala kuwasaidia waovu.
21 Ila atakijaza kinywa chako kicheko,na midomo yako sauti ya furaha.
22 Wale wakuchukiao wataingiwa na aibu,makao ya waovu yatatoweka kabisa.”