Yobu 6 BHN

1 Yobu akamjibu Elifazi:

2 “Laiti mahangaiko yangu yangepimwa uzani wake,mateso yangu yote yakawekwa katika mizani!

3 Yangekuwa mazito kuliko mchanga wa pwani.Ndio maana maneno yangu ni ya kuropoka!

4 Naam, mishale ya Mungu Mwenye Nguvu imenichoma;nafsi yangu imekunywa sumu yake.Vitisho vya Mungu vimenikabili.

5 Je, pundamwitu hulia akiwa na majani,au ng'ombe akiwa na malisho?

6 Je, kitu kisicho na ladha chaweza kuliwa bila chumvi?Je ute wa yai una utamu wowote?

7 Sina hamu ya kuvigusa vyakula hivyo,hivyo ni vyakula vyangu vichukizavyo.”

8 “Laiti ningejaliwa ombi langu,Mungu akanipatia kile ninachotamani:

9 Kwamba angekuwa radhi kunipondaponda,angenyosha mkono wake anikatilie mbali!

10 Hiyo ingekuwa faraja yangu,ningefurahi katika maumivu yasiyo na huruma.

11 Lakini sina nguvu ya kuweza kuendelea;sijui mwisho wangu utakuwaje, nipate kuvumilia.

12 Je, nguvu zangu ni kama za mawe?Au mwili wangu kama shaba?

13 Kweli kwangu hamna cha kunisaidia;msaada wowote umeondolewa kwangu.

14 “Anayekataa kumhurumia rafiki yake,anakataa kumcha Mungu mwenye nguvu.

15 Rafiki zangu wamenidanganya kama kijito,wamenihadaa kama mitaro isiyo na maji.

16 Ambayo imejaa barafu,na theluji imejificha ndani yake.

17 Lakini wakati wa joto hutoweka,wakati wa hari hubaki mito mikavu.

18 Misafara hupotea njia wakitafuta maji,hupanda nyikani na kufia huko.

19 Misafara ya Tema hutafuta tafuta,wasafiri wa Sheba hutumaini.

20 Huchukizwa kwa kutumaini bure,hufika kwenye vijito hivyo na kuudhika.

21 Nyinyi mmekuwa kama vijito hivyo,mwaona balaa yangu na kuogopa.

22 Je, nimesema mnipe zawadi?Au mnitolee rushwa kwa mali zenu?

23 Au mniokoe makuchani mwa adui?Au mnikomboe mkononi mwa wadhalimu?

24 “Nifundisheni, nami nitanyamaza.Nielewesheni jinsi nilivyokosea.

25 Maneno ya kweli yana nguvu kubwa!Lakini makaripio yenu yananikosoa nini?

26 Je, mnadhani kwamba mwaweza kuyakosoa maneno?Maneno ya mtu aliyekata tamaa ni upepo tu.

27 Nyinyi mnathubutu hata kuwapigia yatima kura;mnawapigia bei hata marafiki zenu!

28 Lakini sasa niangalieni tafadhali.Mimi sitasema uongo mbele yenu.

29 Acheni tafadhali, kusiwe na uovu;acheni sasa, kwani mimi ni mnyofu.

30 Je, mnadhani kwamba nimesema uovu?Je, mnafikiri mimi siyatambui machungu?