Yobu 37 BHN

1 “Kutokana na hayo, moyo wangu unatetemeka,na kuruka kutoka mahali pake.

2 Sikilizeni ngurumo ya sauti ya Mungu,na mvumo wa sauti kutoka kinywani mwake.

3 Huufanya uenee chini ya mbingu yote,umeme wake huueneza pembe zote za dunia.

4 Ndipo sauti yake hunguruma,sauti ya Mungu hunguruma kwa faharina muda huo wote umeme humulikamulika.

5 Mungu hupiga radi ya ajabu kwa sauti yake,hufanya mambo makuu tusiyoweza kuyaelewa.

6 Huiambia theluji, ‘Anguka juu ya nchi!’Na manyunyu na mvua, ‘Nyesha kwa nguvu.’

7 Hufunga shughuli za kila mtu;ili watu wote watambue kazi yake.

8 Wanyama wa porini hurudi mafichoni mwao,na hubaki katika mapango yao.

9 Dhoruba huvuma kutoka chumba chake,na baridi kali kutoka ghalani mwake.

10 Kwa pumzi ya Mungu barafu hutokea,uso wa maji huganda kwa haraka.

11 Mungu hulijaza wingu manyunyu mazito;mawingu husambaza umeme wake.

12 Kwa amri yake vyote huzunguka huku na huko,kutekeleza kila kitu anachokiamuru,kufanyika katika ulimwengu wa viumbe.

13 Mungu hutekeleza matakwa yake duniani;iwe ni kwa ajili ya kuwaadhibu watu,au kwa ajili ya kuonesha upendo wake.

14 “Unapaswa kusikiliza Yobu;nyamaza, usikilize maajabu ya Mungu.

15 Je, wajua jinsi Mungu anavyovipa amri yake,na kufanya umeme wa mawingu yake ungae?

16 Je, wajua jinsi mawingu yanavyoelea angani?Ndizo kazi za ajabu za yule aliye mkamilifu wa maarifa!

17 Wewe wajiona umevaa nguo za joto sana,wakati upepo wa kusi unaivamia nchi.

18 Je, waweza, kuzitandaza mbingu kama yeyezikawa ngumu kama kioo cha shaba?

19 Tufundishe tutakachomwambia Mungu;maana hoja zetu si wazi, tumo gizani.

20 Je, nani anathubutu kumwambia: Nataka kuongea?Nani aseme apate balaa?

21 “Ghafla mtu hawezi tena kuona waziwazi:Jua limefichika nyuma ya mawingu,na upepo umefagia anga!

22 Mngao mzuri hutokea kaskazini;Mungu amezungukwa na utukufu wa kutisha.

23 Mungu Mwenye Nguvu asiyeweza kufikiwa na mtu,uwezo na uadilifu wake ni mkuu,amejaa wema wala hapotoshi haki kamwe.

24 Kwa hiyo, watu wote humwogopa;yeye hamjali mtu yeyote mwenye kiburi.”