1 Kisha Elihu akaendelea kusema:
2 “Sikilizeni maneno yangu enyi wenye hekima,nitegeeni masikio yenu, nyinyi wenye ujuzi.
3 Sikio huyapima maneno,kama vile ulimi uonjavyo chakula.
4 Basi, na tuchague lililo sawa,tuamue miongoni mwetu lililo jema.
5 Basi, Yobu ametamka: ‘Mimi Yobu sina hatia,Mungu ameniondolea haki yangu.
6 Ingawa sina hatia naonekana kuwa mwongo;kidonda changu hakiponyeki ingawa sina kosa.’
7 Ni nani aliye kama Yobuambaye kwake ubaradhuli ni kama kunywa maji?
8 Huandamana na watenda maovuhutembea na watu waovu.
9 Maana amesema, ‘Mtu hapati faida yoyote,kujisumbua kumpendeza Mungu.’
10 “Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye ujuzi.Mungu kamwe hawezi kufanya uovu;Mungu Mwenye Nguvu hawezi kufanya kosa.
11 Mungu atamlipa mtu kadiri ya matendo yake,atamlipiza kulingana na mwenendo wake.
12 Ni ukweli mtupu: Mungu hafanyi ovu;Mungu Mwenye Nguvu kamwe hapotoshi haki.
13 Je, kuna aliyemkabidhi mamlaka juu ya dunia?Uwezo wake juu ya ulimwengu ni wake peke yake.
14 Kama Mungu angejifikiria tu yeye mwenyewe,akiondoa pumzi yake ya uhai duniani,
15 viumbe vyote vingeangamia kabisa,naye binadamu angerudi mavumbini.
16 “Kama una akili sikiliza;sikiliza ninachokuambia.
17 Je, anayetawala ulimwengu kwa sheria zake anachukia haki?Je, utathubutu kumhukumu mwadilifu na mwenye nguvu?
18 Amwambiaye mfalme, ‘Wewe ni takataka!’Na watu mashuhuri, ‘Nyinyi ni waovu!’
19 Yeye hawapendelei wakuu,wala kuwajali matajiri kuliko maskini,maana wote hao ni kazi ya mikono yake.
20 Kufumba na kufumbua hao wamekufa;hutikiswa usiku na kuaga dunia;nao wenye nguvu hufutiliwa mbali bila kutumia nguvu za mtu.
21 “Macho ya Mungu huchunguza mienendo ya watu;yeye huziona hatua zao zote.
22 Hakuna weusi wala giza neneambamo watenda maovu waweza kujificha.
23 Mungu hahitaji kumjulisha mtuwakati wa kumleta mbele ya mahakama yake.
24 Huwaangamiza wenye nguvu bila uchunguzi,na kuwaweka wengine mahali pao.
25 Kwa kuwa anayajua matendo yao yote,huwaporomosha usiku wakaangamia.
26 Huwachapa hadharani kwa ajili ya uovu wao,
27 kwa sababu wameacha kumfuata yeye,wakazipuuza njia zake zote.
28 Hata wakasababisha kilio cha maskini kimfikie Mungu,Mungu akasikiliza kilio chao hao walioteswa.
29 Kama Mungu akinyamaza, nani awezaye kumlaumu?Kama akificha uso wake, nani awezaye kumwona,
30 liwe ni taifa au mtu mmojammoja?Hufanya hivyo, mtu mbaya asitawale,au wale wahatarishao maisha ya watu.
31 “Tuseme mtu amemwambia Mungu,‘Nimekosa, sitatenda dhambi tena.
32 Nioneshe makosa nisiyoweza kuyaonakama nimetenda mabaya sitayarudia tena.’
33 Je, Mungu atapaswa kumwadhibu kama uonavyo wewe?Wewe ndiwe unayeamua, sio mimi.Basi, sema unachofikiri wewe.
34 Mtu yeyote mwenye akili,na kila mwenye hekima anayenisikiliza atasema:
35 ‘Yobu anaongea bila kutumia akili,maneno yake hayana maana.’
36 Laiti Yobu angechunguzwa mpaka mwisho,kwa maana anajibu kama watu waovu.
37 Huongeza uasi juu ya dhambi zake;anaeneza mashaka kati yetu,na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”