1 “Sasa, Yobu, sikiliza hoja yangu;sikiliza maneno yangu yote.
2 Tazama, nafumbua kinywa changu,naam, ulimi wangu utasema.
3 Nitasema kadiri ya unyofu wa moyo wangu;ninayoyajua nitayasema kwa uaminifu.
4 Roho ya Mungu iliniumba,nayo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu yanipa uhai.
5 Nijibu, kama unaweza.Panga hoja zako vizuri mbele yangu,ushike msimamo wako.
6 Wewe na mimi ni sawa mbele ya Mungu;mimi pia niliumbwa kwa sehemu ya udongo.
7 Kwa hiyo huna sababu ya kuniogopa;maneno yangu mazito hayatakulemea.
8 Kweli umesema, nami nikasikia;nimeyasikia yote uliyosema.
9 Wewe umesema, u safi na wala huna kosa,u safi kabisa na huna hatia;
10 umesema kwamba Mungu anakutafutia kisa,na kukuona kama adui yake.
11 Anakufunga miguu minyororo,na kuchunguza hatua zako zote.
12 “Lakini Yobu, nakuambia hapo umekosea.Mungu ni mkuu kuliko binadamu.
13 Kwa nini unashindana naye,ukisema hatajibu swali lako moja?
14 Mungu anaposema hutumia njia moja,au njia nyingine lakini mtu hatambui.
15 Mungu huongea na watu katika ndoto na maono,wakati usingizi mzito unapowavamia,
16 wanaposinzia vitandani mwao.Hapo huwafungulia watu masikio yao;huwatia hofu kwa maonyo yake,
17 wapate kuachana na matendo yao mabaya,na kuvunjilia mbali kiburi chao.
18 Hivyo humkinga mtu asiangamie shimoni,maisha yake yasiangamie kwa upanga.
19 “Mungu humrudi mtu kwa maumivu yamwekayo kitandani,maumivu hushika viungo vyake bila kukoma;
20 naye hupoteza hamu yote ya chakula,hata chakula kizuri humtia kinyaa.
21 Mwili wake hukonda hata asitambuliwe,na mifupa yake iliyofichika ikatokeza nje.
22 Yuko karibu sana kuingia kaburini,na maisha yake karibu na wale waletao kifo.
23 Lakini malaika akiwapo karibu naye,mmoja kati ya maelfu ya watetezi wa Mungu,ili kumwonesha lililo jema la kufanya,
24 akamwonea huruma na kumwambia Mungu;‘Mwokoe asiingie Shimoni,ninayo fidia kwa ajili yake.’
25 Hapo mwili wake utaweza kuwa tena kama kijana,ataweza kurudia tena nguvu zake za ujana.
26 Kisha atamwomba Mungu na kukubaliwa,atakuja mbele yake kwa furaha,na Mungu atamrudishia fahari yake.
27 Atashangilia mbele ya watu na kusema:‘Nilitenda dhambi na kupotosha haki,nami sikuadhibiwa kutokana na hayo.
28 Mungu aliniokoa nisiangamie Shimoni;nimebaki hai na ninaona mwanga.’
29 “Tazama Mungu humfanyia binadamu haya yote,tena mara mbili, mara tatu.
30 Humwokoa binadamu asiangamie Shimoni,aweze kuona mwanga wa maisha.
31 Sikia Yobu, nisikilize kwa makini;kaa kimya, nami nitasema.
32 Kama una la kusema, nijibu;sema, maana nataka kukuona huna hatia.
33 La sivyo, nyamaza unisikilize,kaa kimya nami nikufunze hekima.”