1 Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu:
2 “Je, mtu wa hekima hujibu kwa maneno ya upuuzi?Je, mtu huyo amejaa maneno matupu?
3 Je, mwenye hekima hujitetea kwa maneno yasiyofaa,au kwa maneno yasiyo na maana?
4 Lakini wewe unapuuza uchaji wa Mungu;na kuzuia kutafakari mbele ya Mungu.
5 Uovu wako ndio unaokifundisha kinywa chako,nawe wachagua kusema kama wadanganyifu.
6 Maneno yako mwenyewe yanakuhukumu, sio mimi;matamshi yako yashuhudia dhidi yako.
7 Je, wewe ni mtu wa kwanza kuzaliwa?Je, wewe ulizaliwa kabla ya kuweko vilima?
8 Je, ulipata kuweko katika halmashauri ya Mungu?au, wewe ndiwe peke yako mwenye hekima?
9 Unajua kitu gani tusichokijua sisi?Unafahamu kitu gani tusichokifahamu sisi?
10 Miongoni mwetu wapo wazee wenye hekima,wenye miaka mingi kuliko baba yako.
11 Je, faraja anazokupa Mungu ni ndogo mno?Au je, neno lake la upole kwako si kitu?
12 Mbona moyo unakusukuma kukasirikana kutoa macho makali,
13 hata kumwasi Munguna kusema maneno mabaya kama hayo?
14 Mtu ni nini hata aweze kuwa mwadilifu?au yule aliyezaliwa na mwanamke hata aweze kuwa mwema?
15 Ikiwa Mungu hawaamini hata watakatifu wake,nazo mbingu si safi mbele yake,
16 sembuse binadamu aliye kinyaa na mpotovubinadamu atendaye uovu kama kunywa maji!
17 “Sasa nisikilize, nami nitakuonesha,nitakuambia yale niliyoyaona,
18 mafundisho ya wenye hekima,mambo ambayo wazee wao hawakuyaficha,
19 ambao Mungu aliwapa hiyo nchi peke yao,wala hakuna mgeni aliyepita miongoni mwao.
20 Mwovu atateseka kwa maumivu siku zote,miaka yote waliyopangiwa wakatili.
21 Sauti za vitisho zitampigia kelele masikioni,anapodhani amestawi mwangamizi atamvamia.
22 Mwovu hana tumaini la kutoka gizani;mwisho wake ni kufa kwa upanga.
23 Hutangatanga kutafuta chakula,akisema, ‘Kiko wapi?’Ajua kwamba siku ya giza inamkaribia.
24 Taabu na uchungu, vyamtisha;vyamkabili kama jeshi la mfalme anayeshambulia.
25 Kwa sababu amenyosha mkono wake dhidi ya Mungu;akadiriki kumpinga huyo Mungu mwenye nguvu;
26 alikimbia kwa kiburi kumshambulia,huku ana ngao yenye mafundo makubwa.
27 Uso wake ameunenepesha kwa mafuta,na kiuno chake kimejaa mafuta.
28 Ameishi katika miji iliyoachwa tupu,katika nyumba zisizokaliwa na mtu;nyumba zilizotakiwa ziwe lundo la uharibifu.
29 Mtu huyo kamwe hatakuwa tajiri;wala utajiri wake hautadumu duniani.
30 Hatalikwepa giza la kifo.Ndimi za moto zitakausha chipukizi zake,maua yake yatapeperushwa na upepo.
31 Heri aache kutumainia upuuzi na kujidanganya,maana upuuzi ndio utakaokuwa tuzo lake.
32 Atalipwa kikamilifu kabla ya kufa kwake,na wazawa wake hawatadumu.
33 Atakuwa kama mzabibu unaopukutisha zabibu mbichi,kama mzeituni unaoangusha maua yake.
34 Wote wasiomcha Mungu hawatapata watoto,moto utateketeza mahema ya wala rushwa.
35 Wanatunga udanganyifu na kuzaa uovu.Mioyo yao hupanga udanganyifu.”