Yobu 4 BHN

Hoja ya Elifazi

1 Kisha Elifazi yule Mtemani akamjibu Yobu:

2 “Je, mtu akijaribu kukuambia neno utakasirika?Lakini nani awezaye kujizuia kusema?

3 Sikiliza! Wewe umewafundisha wengi,na kuiimarisha mikono ya wanyonge.

4 Maneno yako yamewainua waliokufa moyo,umewaimarisha waliokosa nguvu.

5 Lakini sasa yamekupata, nawe ukakosa subira,yamekugusa, nawe ukafadhaika.

6 Je, kumcha Mungu si ndilo tegemeo lako?Na unyofu wako si ndilo tumaini lako?

7 Fikiri sasa: Nani asiye na hatia ambaye amepata kuangamia?Au, je, waadilifu wamepata kutupwa?

8 Nijuavyo mimi, wapandao uovu na ubaya huvuna hayohayo,

9 Mungu huwaangamiza hao kwa pumzi yake,hao huteketezwa kwa pigo la hasira yake.

10 Waovu hunguruma kama simba mkali,lakini meno yao huvunjwa.

11 Simba mwenye nguvu hufa kwa kukosa mawindo,na watoto wa simba jike hutawanywa!

12 “Siku moja, niliambiwa neno kwa siri,sikio langu lilisikia mnongono wake.

13 Nikiwa katika mawazo ya njozi za usiku,wakati usingizi mzito huwashika watu,

14 nilishikwa na hofu na kutetemeka,mifupa yangu yote ikagonganagongana.

15 Upepo ukapita mbele ya uso wangu,nywele za mwilini mwangu zikajisimamisha.

16 Kitu kilisimama tuli mbele yangu,nilipokitazama sikukitambua kabisa.Kulikuwa na umbo fulani mbele yangu;kulikuwa kimya, kisha nikasikia sauti.

17 Binadamu afaye aweza kuwa mwadilifu mbele ya Mungu?Mtu aweza kuwa safi mbele ya Muumba wake?

18 Hata watumishi wake, Mungu hana imani nao;na malaika wake huwaona wana kosa;

19 sembuse binadamu viumbe vya udongo,watu ambao chanzo chao ni mavumbi,ambao waweza kupondwapondwa kama nondo!

20 Binadamu kwa masaa machache tu waweza kuangamia;huangamia milele bila kuacha hata alama yao!

21 Iwapo uzi unaoshikilia uhai wao ukikatwawao hufa tena bila kuwa na hekima.