1 “Ita sasa, uone kama kuna wa kukuitikia.Ni yupi kati ya watakatifu utakayemwita?
2 Ama kweli hangaiko humuua mpumbavu,na wivu humwangamiza mjinga.
3 Nimepata kuona mpumbavu akifana,lakini ghafla nikayalaani makao yake.
4 Watoto wake hawana usalama;hudhulumiwa mahakamani,na hakuna mtu wa kuwatetea.
5 Mazao yake huliwa na wenye njaa,hata nafaka iliyoota kati ya miiba;wenye tamaa huuonea shauku utajiri wake.
6 Kwa kawaida mateso hayatoki mavumbiniwala matatizo hayachipui udongoni.
7 Bali binadamu huzaliwa apate taabu,kama cheche za moto zirukavyo juu.
8 “Kama ningekuwa wewe ningemgeukia Mungu,ningemwekea yeye Mungu kisa changu,
9 yeye atendaye makuu yasiyochunguzika,atendaye maajabu yasiyohesabika.
10 Huinyeshea nchi mvua,hupeleka maji mashambani.
11 Huwainua juu walio wanyonge,wenye kuomboleza huwapa usalama.
12 Huvunja mipango ya wenye hila,matendo yao yasipate mafanikio.
13 Huwanasa wenye hekima kwa werevu wao,mipango ya wajanja huikomesha mara moja.
14 Hao huona giza wakati wa mchana,adhuhuri hupapasapapasa kama vile usiku.
15 Lakini Mungu huwaokoa yatima wasiuawe,huwanyakua fukara mikononi mwa wenye nguvu.
16 Hivyo maskini wanalo tumaini,nao udhalimu hukomeshwa.
17 “Heri mtu yule ambaye Mungu anamrudi!Hivyo usidharau Mungu Mwenye Nguvu anapokuadhibu.
18 Kwani yeye huumiza na pia huuguza;hujeruhi, na kwa mkono wake huponya.
19 Atakuokoa katika maafa zaidi ya mara moja;katika balaa la mwisho, uovu hautakugusa.
20 Wakati wa njaa atakuokoa na kifo,katika mapigano makali atakuokoa.
21 Utakingwa salama na mashambulio ya ulimi,wala hutaogopa maangamizi yajapo.
22 Maangamizi na njaa vijapo, utacheka,wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.
23 Nawe utaafikiana na mawe ya shambani,na wanyama wakali watakuwa na amani nawe.
24 Utaona nyumbani mwako mna usalama;utakagua mifugo yako utaiona yote ipo.
25 Utaona pia wazawa wako watakuwa wengi,wengi kama nyasi mashambani.
26 Utafariki ukiwa mkongwe mtimilifu,kama mganda wa ngano ya kupurwa iliyoiva vizuri.
27 Basi huu ndio utafiti wetu; tena ni ukweli;uusikie na kuuelewa kwa faida yako.”