1 Kisha Yobu akajibu:
2 “Kweli najua hivyo ndivyo ilivyo.Lakini mtu awezaje kuwa mwema mbele ya Mungu?
3 Kama mtu angethubutu kushindana naye,hataweza kufika mbali;hata kujibu swali moja kati ya elfu.
4 Yeye ni mwenye hekima mno na nguvu nyingi,nani aliyepingana naye, akashinda?
5 Yeye huiondoa milima bila yenyewe kutambua,huibomolea mbali kwa hasira yake.
6 Yeye huitikisa dunia kutoka mahali pake,na nguzo zake zikatetemeka.
7 Huliamuru jua lisichomozehuziziba nyota zisiangaze.
8 Yeye peke yake alizitandaza mbingu,na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9 Ndiye aliyezifanya nyota angani:Dubu, Orioni, Kilimia, na nyota za kusini.
10 Ndiye atendaye makuu yasiyoeleweka,mambo ya ajabu yasiyo na idadi.
11 Loo! Hupita karibu nami nisimwone,kisha huenda zake bila ya mimi kumtambua.
12 Tazama! Yeye huchukua anachotaka;nani awezaye kumzuia?Nani awezaye kumwuliza: ‘Unafanya nini?’
13 “Mungu hatazuia hasira yake;chini yake wainama kwa hofu Rahabu na wasaidizi wake.
14 Nitawezaje basi kumjibu Mungu?Nitachagua wapi maneno ya kumwambia?
15 Ingawa sina hatia, siwezi kumjibu.Lazima kumwomba anihurumie huyo mshtaki wangu.
16 Hata kama ningemwita naye akajibu,nisingeweza kuamini kuwa ananisikiliza.
17 Yeye huniponda kwa dhoruba;huongeza majeraha yangu bila sababu.
18 Haniachi hata nipumue;maisha yangu huyajaza uchungu.
19 Kama ni kushindana, yeye ana nguvu mno!Na kama ni kutafuta juu ya haki,nani atakayemleta mahakamani?
20 Ingawa sina hatia, maneno yangu yenyewe yangenihukumu;ingawa sina lawama, angenithibitisha kuwa mpotovu.
21 Sina lawama, lakini sijithamini.Nayachukia maisha yangu.
22 Yote ni mamoja, kwa hiyo nasema;Mungu huwaangamiza wema na waovu.
23 Maafa yaletapo kifo cha ghafla,huchekelea balaa la wasio na hatia.
24 Nchi ikitiwa watu waovu katika utawala wa mwovu,Mungu huyafumba macho ya mahakimu wake!Kama si yeye afanyaye hivyo, ni nani basi?
25 “Siku zangu zaenda mbio kuliko mpiga mbio;zinakimbia bila kuona faida.
26 Zapita kasi kama mashua ya matete;kama tai anayerukia mawindo yake.
27 Nasema: ‘Nitasahau lalamiko langu,niondoe uso wangu wa huzuni na kuwa na furaha!’
28 Lakini nayaogopa maumivu yangu yote,kwani najua Mungu hataniona kuwa sina hatia.
29 Ikiwa nitahukumiwa kuwa na hatia,ya nini basi nijisumbue bure?
30 Hata kama nikitawadha kwa theluji,na kujitakasa mikono kwa sabuni,
31 hata hivyo, atanitumbukiza shimoni kwenye uchafu,na mavazi yangu yataniona kuwa kinyaa.
32 Mungu si mtu kama mimi niweze kumjibu,hata tuweze kwenda mahakamani pamoja.
33 Hakuna msuluhishi kati yetu,ambaye angeamua kati yetu sisi wawili.
34 Mungu na aniondolee hiyo fimbo ya kunipiga,na kitisho chake kisinitie hofu!
35 Hapo ningeweza kusema bila kumwogopa;kwani sivyo nilivyo nafsini mwangu.