7 Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Yobu, alimwambia Elifazi, Mtemani, “Ghadhabu yangu imewaka dhidi yako na marafiki zako wawili kwani hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Yobu alivyofanya.
8 Kwa hiyo chukueni mafahali saba na kondoo madume saba, mwende kwa mtumishi wangu Yobu, mkawatoe sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yenu. Naye mtumishi wangu Yobu atawaombeeni, nami nitaisikiliza sala yake na kuacha kuwatenda kulingana na upumbavu wenu; maana hamkusema ukweli juu yangu kama mtumishi wangu Yobu alivyofanya.”
9 Basi, Elifazi Mtemani, Bildadi, Mshua na Sofari Mnaamathi, wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaambia. Mwenyezi-Mungu akaipokea sala ya Yobu.
10 Baada ya Yobu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi-Mungu akamrudishia Yobu hali yake ya kwanza. Alimpa maradufu ya yote aliyokuwa nayo hapo awali.
11 Kisha ndugu zake, dada zake na rafiki wote waliomfahamu hapo awali wakamwendea nyumbani kwake, wakala chakula pamoja naye. Wakampa pole na kumfariji kwa ajili ya mateso yote ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemletea. Kila mmoja wao akampa Yobu fedha na pete ya dhahabu.
12 Katika miaka ya Yobu iliyofuata Mwenyezi-Mungu alimbariki zaidi kuliko hata alivyokuwa amembariki pale awali. Basi Yobu akawa na kondoo 14,000, ngamia 6,000, ng'ombe 2,000 na punda majike 1,000.
13 Alikuwa pia na watoto wa kiume saba na wa kike watatu.