Isaya 3 BHN

Msukosuko Yerusalemu

1 Sasa, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshiataondoa kutoka Yerusalemu na Yuda kila tegemeo:Tegemeo lote la chakula,na tegemeo lote la kinywaji.

2 Ataondoa mashujaa na askari,waamuzi na manabii,waaguzi na wazee,

3 majemadari wa vikosi vya watu hamsini,na watu wenye vyeo,washauri, wachawi stadi na walozi hodari.

4 Mungu ataweka watoto wawatawale;naam, watoto wachanga watawatawala.

5 Watu watadhulumiana,kila mtu na jirani yake;vijana watawadharau wazee wao,na watu duni watapuuza wakuu wao.

6 Wakati huo ndugu atamwambia ndugu yakewakiwa bado nyumbani kwa baba yao:“Wewe unalo koti;utakuwa kiongozi wetu.Chukua hatamu juu ya uharibifu huu!”

7 Lakini siku hiyo atasema,“Mimi siwezi kuwa mwuguzi,nyumbani mwangu hamna chakula wala mavazi.Msinifanye mimi kuwa kiongozi wenu.”

8 Watu wa Yerusalemu wamejikwaa,watu wa Yuda wameanguka,kwa kuwa wanampinga Mwenyezi-Mungukwa maneno na matendo,wakipuuza utukufu wake miongoni mwao.

9 Ubaguzi wao unashuhudia dhidi yao;wanatangaza dhambi yao kama ya Sodoma,wala hawaifichi.Ole wao watu hao,kwani wamejiletea maangamizi wenyewe.

10 Waambieni waadilifu jinsi walivyo na bahati:Kwani watakula matunda ya matendo yao.

11 Lakini ole wao watu waovu!Mambo yatawaendea vibaya,kwani waliyotenda yatawapata wao wenyewe.

12 Watu wangu watadhulumiwa na watoto;wanawake ndio watakaowatawala.Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,wanavuruga njia mnayopaswa kufuata.

Mwenyezi-Mungu awahukumu watu wake

13 Mwenyezi-Mungu yu tayari kuanza mashtaka,anasimama kuwahukumu watu wake.

14 Mwenyezi-Mungu anawashtakiwazee na wakuu wa watu wake:“Nyinyi ndio mlioliharibu shamba la mizabibu;mali walizowanyanganywa maskini zimo nyumbani kwenu.

15 Mnamaanisha nini kuwakandamiza watu wangu,kuwatendea ukatili watu maskini?Nauliza mimi Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”

Onyo kwa wanawake wa Yerusalemu

16 Mwenyezi-Mungu asema:“Wanawake wa Siyoni wana kiburi;wanatembea wameinua shingo juu,wakipepesa macho yao kwa tamaa.Hatua zao ni za maringo,na miguuni njuga zinalia.

17 Basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitawaadhibu;nitawanyoa nywele hao wanawake wa Siyoni,na kuwavua nguo za kufunika uchi wao.”

18 Siku yaja ambapo Mwenyezi-Mungu atawanyanganya wanawake wa Yerusalemu vitu vyote wanavyoringia: Njuga, kaya, mikufu,

19 vipuli, vikuku, shungi,

20 vitambaa vya kichwani, bangili, vibwebwe, vibweta vya marashi, hirizi,

21 pete, hazama,

22 mavazi ya sikukuu, mitandio, majoho, mikoba,

23 mavazi yaoneshayo, mavazi ya kitani, vilemba na shela.

24 Badala ya kunukia marashi watatoa uvundo;badala ya mishipi mizuri watatumia kamba;badala ya nywele nzuri watakuwa na upara;badala ya mavazi mazuri watavaa matambara;uzuri wao wote utageuka kuwa aibu.

25 Wanaume wenu wataangamia kwa upanga,watu wenu wenye nguvu watakufa vitani.

26 Malango ya mji yatalia na kuomboleza;nao mji utakuwa kama mwanamke aliyepokonywa kila kitu, ameketi mavumbini.