Isaya 5 BHN

Wimbo wa shamba la mizabibu

1 Nitaimba juu ya rafiki yangu,wimbo wa rafiki yangu na shamba lake la mizabibu:Rafiki yangu alikuwa na shamba la mizabibujuu ya kilima chenye rutuba nyingi.

2 Alililima vizuri na kuondoa mawe yote,akaotesha humo mizabibu iliyochaguliwa;alijenga mnara wa ulinzi katikati yake,akachimba kisima cha kusindikia divai.Kisha akangojea lizae zabibu,lakini likazaa zabibu chungu.

3 Kwa hiyo rafiki yangu anasema hivi:“Enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,amueni tafadhali kati yangu na shamba langu.

4 Ni kitu gani nilichokosa kulifanyia shamba langu?Na nilipotazamia lizae zabibu nzuri,mbona basi, likazaa zabibu chungu?

5 “Na sasa nitawaambieninitakavyolifanya hilo shamba langu.Nitauondoa ua wake,nalo litaharibiwa.Nitaubomoa ukuta wake,nalo litakanyagwakanyagwa.

6 Nitaliacha liharibiwe kabisa,mizabibu yake haitapogolewa wala kupaliliwa.Litaota mbigili na miiba.Tena nitayaamuru mawinguyasinyeshe mvua juu yake.”

7 Naam! Shamba la mizabibu la Mwenyezi-Mungu wa majeshini jumuiya ya Waisraeli,na mizabibu mizuri aliyoipanda ni watu wa Yuda.Yeye alitazamia watende haki,badala yake wakafanya mauaji;alitazamia uadilifu,badala yake wakasababisha kilio!

Maovu wanayotenda watu

8 Ole wao wanaonunua nyumba baada ya nyumba,wanaoongeza mashamba juu ya mashamba yao,mpaka kila sehemu inakuwa mali yao,na hamna nafasi kwa wengine nchini.

9 Nimemsikia Mwenyezi-Mungu wa majeshi akitamka hivi:“Hakika nyumba nyingi zitabaki tupu,majumba makubwa mazuri bila wakazi.

10 Shamba la mizabibu la eka kumilitatoa lita nane tu za divai;anayepanda kilo 100 za mbeguatavuna kilo 10 tu za nafaka.”

11 Ole wao wanaoamka asubuhi na mapemawapate kukimbilia kunywa kileo;wanaokesha hata usiku,mpaka divai iwaleweshe!

12 Katika karamu zao, hapakosekani vinubi,zeze, matari, filimbi na divai.Lakini hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu,wala kuzitambua kazi za mikono yake.

13 Kwa hiyo, watu wangu watapelekwa uhamishonikwa sababu ya utovu wao wa akili.Watu wenu mashuhuri watakufa njaa,watu wengi watakufa kwa kiu.

14 Kuzimu inawangoja kwa hamu kubwa,imepanua kinywa chake mpaka mwisho.Waheshimiwa pamoja na raia wa Yerusalemuwanaingia humo makundi kwa makundi,kadhalika na wote wanaousherehekea.

15 Kila mtu atafedheheshwa,na wenye kiburi wote wataaibishwa.

16 Lakini Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatukuzwa.Yeye huonesha ukuu wakekwa matendo yake ya haki,kwa kuwahukumu watu wake.

17 Wanakondoo, wanambuzi na ndama,watapata malisho yao kwenye magofu ya miji yao,kana kwamba hizo ni sehemu za malisho yao.

18 Ole wao wanaoburuta uovu kama kwa kamba;wanaokokota dhambi kama kwa kamba za mkokoteni.

19 Wanasema:“Mwache Mwenyezi-Mungu afanye haraka,tunataka kuyaona aliyosema atayafanya!Mtakatifu wa Israeli na atimize kusudi lake.Hebu na tuone ana mipango gani!”

20 Ole wao wanaosema uovu ni wemana wema ni uovu.Giza wanasema ni mwangana mwanga wanasema ni giza.Kichungu wanasema ni kitamuna kitamu wanakiona kuwa kichungu.

21 Ole wao wanaojiona kuwa wenye hekimaambao wanajiona kuwa wenye akili.

22 Ole wao mabingwa wa kunywa divai,hodari sana wa kuchanganya vileo.

23 Kwa hongo kidogo wanawaachilia wenye hatiana kuwanyima wasio na hatia haki yao.

24 Kwa hiyo, kama moto uteketezavyo nyasi,kama majani yateketeavyo katika mwali wa motondivyo na mizizi yao itakavyooza,na maua yao yatakavyopeperushwa juu kama vumbi.Maana wameiacha sheria ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi,wamedharau neno la yule Mtakatifu wa Israeli.

25 Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwawakia watu wake,akaunyosha mkono wake dhidi yao, akawachapa,hata milima ikatetemeka,maiti zao zikawa kama takatakakatika barabara za mji.Hata hivyo, hasira yake haikutulia,mkono wake bado ameunyosha kuwaadhibu.

26 Mwenyezi-Mungu analiashiria taifa la mbali;anawapigia mruzi watu kutoka miisho ya dunia;nao waja mbio na kuwasili haraka!

27 Hawachoki wala hawajikwai;hawasinzii wala hawalali;hakuna mshipi wao uliolegeawala kamba ya kiatu iliyokatika.

28 Mishale yao ni mikali sana,pinde zao zimevutwa tayari.Kwato za farasi wao ni ngumu kama mawe;mwendo wa magurudumu ya magari ni kimbunga.

29 Askari wao wananguruma kama simba;wananguruma kama wanasimbaambao wamekamata mawindo yaona kuwapeleka mahali mbaliambapo hakuna awezaye kuwanyanganya.

30 Siku hiyo, watanguruma juu ya Israelikama mvumo wa bahari iliyochafuka.Atakayeiangalia nchi kavuataona giza tupu na dhiki,mwanga utafunikwa na mawingu.