1 Sikilizeni, enyi watu wa Yakobo,enyi mnaojulikana kwa jina la Israeli,nyinyi mlio wa ukoo wa Yuda.Nyinyi huapa kwa jina la Mwenyezi-Mungu,na kudai mnamwabudu Mungu wa Israeli;lakini hayo si ukweli wala sawa.
2 Nyinyi mnaona fahari kujiita watu wa mji mtakatifu,na kujidai kumtegemea Mungu wa Israeli,ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
3 “Nilitangaza zamani matukio ya awali,niliyatamka mimi mwenyewena kuyafanya yajulikane kwenu.Mara nikaanza kuyatekeleza,nayo yakapata kutukia.
4 Lakini nilikujua wewe kuwa mkaidi;kichwa kigumu kama chuma,uso wako mkavu kama shaba.
5 Kwa hiyo nilikutangazia tangu zamani,kabla hayajatukia mimi nilikutangazia,usije ukasema, ‘Kinyago changu kiliyatenda hayo,sanamu zangu za kuchonga na kusubu ziliyafanya.’
6 “Wewe uliyasikia na sasa unayaona yote.Kwa nini huwezi kuyakiri?Tangu sasa nitakujulisha mambo mapya;mambo yaliyofichika ambayo hukuyajua.
7 Mambo hayo yanatukia sasa;hukupata kuyasikia kabla ya leo,hivyo huwezi kusema, ‘Aa! Nilikwisha yajua.’
8 Hujapata kamwe kuyasikia wala kuyajua;tangu zamani masikio yako hayakuyasikia.Nilijua kuwa wewe ni mwenye hila,na kwamba wewe ni mwasi tangu kuzaliwa.
9 “Kwa heshima ya jina langu,ninaiahirisha hasira yangu;kwa ajili ya heshima yangu,ninaizuia nisije nikakuangamiza.
10 Mimi nitawajaribu lakini si kama fedha katika tanuri.Nitawajaribu katika tanuri ya taabu.
11 Ninafanya hivyo kwa ajili yangu mwenyewe.Kwa nini jina langu lidharauliwe?Utukufu wangu siwezi kumpa mwingine!
12 “Nisikilize ee taifa la Yakobo,nisikilize ee Israeli niliyekuita.Mimi ndiye Mungu;mimi ni wa kwanza na wa mwisho.
13 Kwa mkono wangu niliuweka msingi wa dunia,mimi mwenyewe nilizitandaza mbingu.Nikiziita mbingu na dunia,zinasimama haraka mbele yangu.
14 “Kusanyikeni nyote msikilize!Nani kati ya miungu yenu aliyetabiri vitu hivi?Mimi Mwenyezi-Mungu nampenda Koreshi;yeye atatekeleza lengo langu kuhusu Babuloni,naam, yeye atawashambulia Wakaldayo.
15 Mimi, naam, mimi nimeyasema na kumwita;nimemleta, naye atafaulu katika mpango wake.
16 Njoni karibu nami msikie jambo hili:Tangu mwanzo mimi sikusema kwa siri,tangu mambo hayo yaanze kutendeka, nimekuwapo.”Sasa, Bwana Mungu amenituma,na kunipa nguvu ya roho yake.
17 Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli,Mkombozi wako, asema hivi:“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,ninayekufundisha kwa faida yako,ninayekuongoza katika njia unayotakiwa kwenda.
18 Laiti ungalizitii amri zangu!Hapo baraka zingekutiririkia kama mto,ungepata fanaka kwa wingi kama mawimbi ya bahari.
19 Wazawa wako wangekuwa wengi kama mchanga,naam, wangekuwa wengi kama chembe za mchanga.Jina lao kamwe lisingaliondolewa,kumbukumbu lao halingalitoweka mbele yangu.”
20 Sasa, ondokeni Babuloni!Kimbieni kutoka Kaldayo!Tangazeni jambo hili kwa sauti za shangwe,enezeni habari zake kila mahali duniani.Semeni: “Mwenyezi-Mungu amelikomboataifa la mtumishi wake Yakobo.”
21 Alipowaongoza jangwani hawakuona kiu,aliwatiririshia maji kutoka mwambani,aliupasua mwamba maji yakabubujika.
22 Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Watu waovu sitawapa amani.”