Isaya 54 BHN

Upendo wa Mungu kwa Israeli

1 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Imba kwa shangwe ewe uliye tasa,wewe ambaye hujapata kuzaa!Paza sauti na kuimba kwa nguvu,wewe usiyepata kujifungua mtoto.Maana watoto wako wewe uliyeachwawatakuwa wengi kuliko wa aliye na mume.

2 Panua nafasi hemani mwako,tandaza mapazia hapo unapoishi,usijali gharama zake.Zirefushe kamba zake,na kuimarisha vigingi vyake;

3 maana utapanuka kila upande;wazawa wako watamiliki mataifa,miji iliyokuwa mahame itajaa watu.

4 Usiogope maana hutaaibishwa tena;usifadhaike maana hutadharauliwa tena.Utaisahau aibu ya ujana wako,wala hutaikumbuka tena fedheha ya ujane wako.

5 Muumba wako atakuwa mume wako;Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina lake,Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako;yeye aitwa ‘Mungu wa ulimwengu wote’.

6 “Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu amekuita tena wewekama vile mke aliyeachwa na kuhuzunika,mke aliyeolewa akiwa kijana akaachwa.Mungu wako anasema:

7 Nilikuacha kwa muda mfupi tu;kwa huruma nyingi, nitakurudisha.

8 Kwa hasira nyingi nilikuficha uso wangu kwa kitambo,lakini kwa fadhili za milele nitakuonea huruma.Mimi Mwenyezi-Mungu Mkombozi wako, nimesema.

9 “Nitafanya kama nilivyofanya wakati wa Noa:Wakati ule niliapa kwambasitaifunika tena ardhi kwa gharika.Basi sasa naapa kwamba sitakukasirikia tenawala sitakukemea tena.

10 Milima yaweza kutoweka,vilima vyaweza kuondolewa,lakini fadhili zangu hazitakuondoka,agano langu la amani halitaondolewa.Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema.

Yerusalemu mpya

11 “Ewe Yerusalemu uliyeteseka,uliyetaabishwa na kukosa wa kukufariji!Nitakujenga upya kwa mawe ya thamani,misingi yako itakuwa ya johari ya rangi ya samawati.

12 Minara yako nitaijenga kwa mawe ya akiki,malango yako kwa almasi,na ukuta wako kwa mawe ya thamani.

13 “Watu wako watafunzwa nami Mwenyezi-Mungu,wanao watapata ustawi mwingi.

14 Utaimarika katika uadilifu,utakuwa mbali na dhuluma,nawe hutaogopa kitu;utakuwa mbali na hofu,maana haitakukaribia.

15 Mtu yeyote akija kukushambulia,hatakuwa ametumwa nami.Yeyote atakayekushambulia,ataangamia mbele yako.

16 “Tazama, mimi ndiye niliyemuumba mhunzi,afukutaye moto wa makaa na kufua silaha.Ni mimi pia niliyemuumba mwangamizi anayeangamiza.

17 Silaha zote zilizoundwa kukudhuru wewehazitafaa chochote kile.Mtu akikushtaki mahakamani, utamshinda.Hilo ndilo fungu nililowapangia watumishi wangu.Hizo ndizo haki nilizowathibitishia.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.