1 Sargoni mfalme wa Ashuru, alimtuma jemadari wake mkuu kuuvamia mji wa Ashdodi. Naye akaushambulia na kuuteka.
2 Miaka mitatu kabla ya hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Isaya, mwana wa Amozi hivi: “Nenda ukavue vazi la gunia unalovaa kiunoni, na viatu miguuni mwako.” Isaya akafanya hivyo; akawa anatembea uchi na bila viatu.
3 Basi, mnamo mwaka huo mji wa Ashdodi ulipotekwa, Mwenyezi-Mungu alisema: “Mtumishi wangu Isaya amekuwa akitembea uchi na bila viatu kwa muda wa miaka mitatu sasa, kama ishara na alama dhidi ya nchi ya Misri na Kushi.
4 Basi, mfalme wa Ashuru atawachukua mateka Wamisri na Wakushi, wakubwa kwa wadogo. Watachukuliwa, nao watatembea uchi na bila viatu; matako wazi, kwa aibu ya Misri.
5 Kisha wote waliotegemea Kushi na kujivunia Misri watajuta na kufadhaika.
6 Wakati huo, wakazi wa pwani ya Filistia watasema, ‘Tazameni yaliyowapata watu tuliowategemea na kuwakimbilia kuomba msaada watuokoe na mfalme wa Ashuru! Na sasa, sisi tutawezaje kusalimika?’”