Isaya 43 BHN

Mungu aahidi kuwaokoa watu wake

1 Mwenyezi-Mungu aliyewaumba enyi watu wa Yakobo,yeye aliyewafanya enyi watu wa Israeli, asema:“Msiogope, maana mimi nimewakomboa;nimewaita kwa jina nanyi ni wangu.

2 Mkipita katika mafuriko,mimi nitakuwa pamoja nanyi;mkipita katika mito,haitawashinda nguvu.Mkitembea katika moto,hamtaunguzwa;mwali wa moto hautawaunguza.

3 Maana mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,Mungu Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wenu.Nitaitoa nchi ya Misri iwe fidia yenu,nitaitoa Kushi na Seba ili mwachwe huru.

4 Kwa vile mna thamani mbele yangu,kwa kuwa nimewapa hadhi na kuwapenda,mimi nawaacha watu kusudi niwapate nyinyi,nayaachilia mataifa badala ya maisha yenu.

5 Msiogope maana mimi nipo pamoja nanyi.“Nitawarudisha wazawa wenu toka mashariki,nitawakusanyeni kutoka magharibi.

6 Nitaiambia kaskazini, ‘Waache waondoke’,na kusini, ‘Usiwazuie’!Warudisheni watu kutoka mbali,kutoka kila mahali duniani.

7 Kila mmoja hujulikana kwa jina langu,niliwaumba wote na kuwafanyakwa ajili ya utukufu wangu.”

Israeli ni ushahidi wa Mwenyezi-Mungu

8 Waleteni mbele watu hao,ambao wana macho lakini hawaoniwana masikio lakini hawasikii!

9 Mataifa yote na yakusanyike,watu wote na wakutane pamoja.Nani kati ya miungu yao awezaye kutangaza yatakayotukia?Nani awezaye kutuonesha yanayotukia sasa?Wawalete mashahidi waokuthibitisha kwamba walifanya hivyo.Waache wasikilize na kusema, “Ilikuwa kweli.”

10 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Nyinyi Waisraeli ni mashahidi wangu;niliwachagua muwe watumishi wangu,mpate kunijua na kuniamini,kwamba ndimi peke yangu Mungu.Kabla yangu hajapata kuwapo mungu mwingine,wala hatakuwapo mungu mwingine.

11 “Mimi peke yangu ndimi Mwenyezi-Mungu,hakuna mkombozi mwingine ila mimi.

12 Nilitangaza yale ambayo yangetukia,kisha nikaja na kuwakomboa.Hakuna mungu mwingine aliyewahi kufanya hivyo,nanyi ni mashahidi wangu.

13 Mimi ni Mungu na nitakuwa Mungu daima.Hakuna awezaye kuiepa nguvu yangu;hakuna awezaye kupinga ninayofanya.”

Kukombolewa kutoka Babuloni

14 Mwenyezi-Mungu, Mkombozi wenu,Mtakatifu wa Israeli, asema hivi:“Kwa ajili yenu nitatuma jeshi Babuloni.Nitayavunjilia mbali malango ya mji wake,na kelele za hao Wakaldayo zitageuka maombolezo.

15 Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wenu;Mimi ndimi Muumba wa Israeli, Mfalme wenu.”

16 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Wakati mmoja nilifanya barabara baharininikaweka njia kati ya mawimbi makubwa.

17 Nililipiga jeshi lenye nguvu,jeshi la magari na farasi wa vita,askari na mashujaa wa vita.Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena,niliwakomesha na kuwazima kama utambi wa taa.Sasa nasema:

18 ‘Msiyanganganie mambo yaliyopita,wala msifikirie vitu vya zamani.

19 Tazameni, mimi ninafanya kitu kipya.Kinafanyika sasa hivi,nanyi mtaweza kukiona.Nitafanya njia nyikani,na kububujisha mito jangwani.

20 Wanyama wa porini wataniheshimu,kina mbweha na kina mbuni,maana nitaweka maji nyikani,na kububujisha mito jangwani,ili kuwanywesha watu wangu wateule,

21 watu niliowaumba kwa ajili yangu mwenyewe,ili wazitangaze sifa zangu!’

Dhambi ya Israeli

22 “Lakini ewe taifa la Yakobo, hukuniabudu mimi;enyi watu wa Israeli, mlinichoka mimi!

23 Hamjaniletea kondoo wenu wa sadaka za kuteketezwa,wala kuniheshimu kwa tambiko zenu.Nami sikuwalemeza kwa kutaka sadaka,wala sikuwachosha kwa kuwadai ubani.

24 Hamkuninunulia manukato kwa faida yenu,wala kuniridhisha kwa nyama nono za tambiko.Badala yake dhambi zenu zimekuwa mzigo kwangu,mmenichosha kabisa kwa makosa yenu.

25 Walakini mimi ndimi niliyefuta makosa yenu kwa heshima yangu,ndimi niyafutaye makosa kwa ajili yangu mwenyewe,na wala sitazikumbuka dhambi zenu.

26 “Niambie kama mna kisa nami,njoo tukahojiane;toeni mashtaka yenu ili tuuone ukweli wenu!

27 Babu yenu wa kwanza alitenda dhambi,wapatanishi wenu waliniasi.

28 Kwa hiyo niliwafanya haramu wakuu wa mahali patakatifunikawaacha watu wa Yakobo waangamizwe,naam, nikawaacha Waisraeli watukanwe.”