1 Nyika na nchi kavu vitachangamka,jangwa litafurahi na kuchanua maua.
2 Litachanua maua kwa wingi kama waridi,litashangilia na kuimba kwa furaha.Mungu atalijalia fahari ya milima ya Lebanoni,uzuri wa mlima Karmeli na wa bonde la Sharoni.Watu watauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu,watauona ukuu wa Mungu wetu.
3 Imarisheni mikono yenu dhaifu,kazeni magoti yenu manyonge.
4 Waambieni waliokufa moyo:“Jipeni moyo, msiogope!Tazameni Mungu wenu atakuja kulipiza kisasi,atakuja kuwaadhibu maadui zenu;atakuja yeye mwenyewe kuwaokoeni.”
5 Hapo vipofu wataona tena,na viziwi watasikia tena.
6 Walemavu watarukaruka kama paa,na bubu wataimba kwa furaha.Maji yatabubujika nyikanina vijito vya maji jangwani.
7 Mchanga wa moto jangwani utakuwa bwawa la maji,ardhi kavu itabubujika vijito vya maji.Makao ya mbwamwitu yatajaa maji;nyasi zitamea na kukua kama mianzi.
8 Humo kutakuwa na barabara kuu,nayo itaitwa “Njia Takatifu.”Watu najisi hawatapitia humo,ila tu watu wake Mungu;wapumbavu hawatadiriki kuikanyaga,
9 humo hakutakuwa na simba,mnyama yeyote mkali hatapitia humo,hao hawatapatikana humo.Lakini waliokombolewa ndio watakaopita humo.
10 Waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu watarudi,watakuja Siyoni wakipiga vigelegele.Watakuwa wenye furaha ya milele,watajaliwa furaha na shangwe;huzuni na kilio vitatoweka kabisa.