1 Amka! Amka!Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni!Jivike mavazi yako mazuri,ewe Yerusalemu, mji mtakatifu.Maana hawataingia tena kwakowatu wasiotahiriwa na walio najisi.
2 Jikungute mavumbi, uinukeewe Yerusalemu uliyetekwa nyara!Jifungue minyororo yako shingoni,ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka.
3 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja.
4 Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote.
5 Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku.
6 Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!”
7 Tazama inavyopendezakumwona mjumbe akitokea mlimani,ambaye anatangaza amani,ambaye analeta habari njema,na kutangaza ukombozi!Anauambia mji wa Siyoni:“Mungu wako anatawala!”
8 Sikiliza sauti ya walinzi wako;wanaimba pamoja kwa furaha,maana wanaona kwa macho yao wenyewe,kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni.
9 Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu!Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake,ameukomboa mji wa Yerusalemu.
10 Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu,mbele ya mataifa yote.Atawaokoa watu wake,na ulimwengu wote utashuhudia.
11 Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa;msiguse kitu chochote najisi!Ondokeni huku Babuloni!Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu.
12 Safari hii hamtatoka kwa haraka,wala hamtaondoka mbiombio!Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni,Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma.
13 Mungu asema hivi:“Mtumishi wangu atafanikiwa;atatukuzwa na kupewa cheo,atapata heshima kuu.
14 Wengi waliomwona walishtuka,kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa;hakuwa tena na umbo la kibinadamu!
15 Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi.Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake,maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa,na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”