Isaya 56 BHN

Wote wanakaribishwa

1 Mwenyezi-Mungu asema:“Zingatieni haki na kutenda mema,maana nitawaokoeni hivi karibuni,watu wataona wazi kwamba ninawakomboeni.

2 Heri mtu anayezingatia kikamilifu ninayosema,anayeshika sheria ya Sabato kwa heshimana kuepa kutenda uovu wowote.

3 “Mgeni anayenitambua mimi Mwenyezi-Mungu asifikiri:‘Hakika Mwenyezi-Mungu atanitenga na watu wake.’Naye towashi asiseme:‘Mimi ni mti mkavu tu!’

4 Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema:Towashi ashikaye sheria zangu za Sabato,anayefanya mambo yanayonipendeza,na kulizingatia agano langu,

5 nitampa nafasi maalumu na ya sifakatika nyumba yangu na kuta zake;nafasi bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:Nitampa jina la kukumbukwa daima,na ambalo halitafutwa kamwe.

6 “Watu wageni watakaonikiri mimi Mwenyezi-Mungu,watakaoniheshimu, wakapenda jina langu na kuwa watumishi wangu,wote watakaoshika Sabato bila kuikufuru,watu watakaozingatia agano langu,

7 hao nitawaleta katika mlima wangu mtakatifu,na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala;tambiko na sadaka zao zitakubaliwa madhabahuni pangu.Maana nyumba yangu itaitwa:‘Nyumba ya sala kwa ajili ya watu wote’.

8 “Hii ni kauli yangu mimi Bwana Mwenyezi-Munguninayewakusanya Waisraeli waliotawanyika.Licha ya hao niliokwisha kukusanya,nitawakusanya watu wengine wajumuike nao.”

Viongozi wa Israeli walaumiwa

9 Enyi wanyama wote wakali,nanyi wanyama wote wa mwituni,njoni muwatafune watu wangu.

10 Maana viongozi wao wote ni vipofu;wote hawana akili yoyote.Wote ni kama mbwa bubu wasiobweka,hulala tu na kuota ndoto,hupenda sana kusinzia!

11 Hao ni kama mbwa wenye uchu sana,wala hawawezi kamwe kutoshelezwa.Wachungaji hao hawana akili yoyote;kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.

12 Huambiana, “Njoni, twende kutafuta divai;njoni tunywe tushibe pombe!Kesho itakuwa kama leo,tena itakuwa sikukuu kubwa zaidi.”