1 Ole wako Yerusalemu, madhabahu ya Mungu;mji ambamo Daudi alipiga kambi yake!Miaka yaja na kupita,na sikukuu zako zaendelea kufanyika;
2 lakini mimi Mungu nitauhuzunisha Yerusalemu,nako kutakuwa na vilio na maombolezo,mji wenyewe utakuwa kama madhabahuiliyolowa damu ya watu waliouawa.
3 Mimi nitapanga jeshi dhidi ya Yerusalemu,nami nitauzingira na kuushambulia.
4 Utaangushwa mbali sana ndani ya ardhi;kutoka huko mbali utatoa sauti;maneno yako yatatoka huko chini mavumbini;sauti yako itatoka ardhini kama ya mzimu.
5 Kundi la maadui zako litakuwa kama vumbi laini,waliokutendea ukatili watakuwa kama makapi.Hayo yatafanyika ghafla.
6 Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuja kukusaidia;atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi na sauti kubwa;atakuja na kimbunga, tufani na moto uunguzao.
7 Hapo, kundi la mataifa yote yanayoshambulia Yerusalemu,wote wanaoshambulia ngome yake na kuutia wasiwasi,watatoweka kama ndoto, kama maono ya usiku.
8 Mataifa yote yanayoushambulia mji wa Yerusalemuyatakuwa kama mtu mwenye njaa anayeota anakulalakini aamkapo bado anaumwa na njaa!Au mtu mwenye kiu anayeota kuwa anakunywa,lakini anaamka mdhaifu, bado ana kiu.
9 Endeleeni kuwa wapumbavu na kuduwaa!Jipofusheni na kuwa vipofu!Leweni lakini si kwa divai;pepesukeni lakini si kwa pombe.
10 Mwenyezi-Mungu amewamiminia hali ya usingizi mzito;ameyafumba macho yenu enyi manabii,amefunika vichwa vyenu enyi waonaji.
11 Basi, kwenu nyinyi maono yote haya ni kama ujumbe ulioandikwa katika kitabu kilichofungwa kwa mhuri. Ukimpelekea mtu yeyote ajuaye kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atasema, “Siwezi kukisoma kwani kimefungwa kwa mhuri.”
12 Na ukimpa mtu yeyote asiyejua kusoma, ukamwambia, “Hebu nisomee kitabu hiki,” atakuambia, “Sijui kusoma.”
13 Bwana asema,“Watu hawa huja kuniabudu kwa maneno matupu,hali mioyo yao iko mbali nami.Wananiheshimu kulingana na mapokeo ya watu tu,jambo walilojifunza wao wenyewe.
14 Hivyo, nitawatenda tena watu hawa maajabu,mambo ya ajabu na ya kushangaza.Nao wenye hekima wao wataishiwa hekima,na busara ya wenye busara wao itatoweka.
15 “Ole mnaomficha Mwenyezi-Mungu mipango yenu,mnaotenda matendo yenu gizanina kusema: ‘Hamna atakayetuona;nani awezaye kujua tunachofanya?’
16 Nyinyi mnafanya mambo kinyume kabisa!Je, mfinyanzi na udongo ni hali moja?Chombo hakiwezi kumwambia aliyekitengeneza:‘Wewe hukunitengeneza.’Kilichofinyangwa hakiwezi kumwambia aliyekiumba,‘Wewe hujui chochote.’”
17 Bado kidogo tu,msitu wa Lebanoni utageuzwa kuwa shamba lenye rutuba,na shamba lenye rutuba kuwa msitu.
18 Siku hiyo viziwi watasikia ujumbe ukisomwa kitabunina kutoka gizani vipofu wataanza kuona.
19 Wanyofu watapata furaha mpya kwa Mwenyezi-Mungu,na maskini wa watu watashangilia kwa furahakwa sababu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli.
20 Majitu makatili yataangamizwa,wenye kumdhihaki Mungu watakwisha,wote wanaootea kutenda maovu watatokomezwa.
21 Watatoweka wale wanaopotosha kesi ya mtu mahakamani,watu wanaowafanyia hila mahakimuna wasemao uongo kuwanyima haki yao wasio na hatia.
22 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu aliyemkomboa Abrahamu,asema hivi kuhusu wazawa wa Yakobo:“Wazawa wa Yakobo hawataaibishwa tena,hawatainamisha vichwa vyao tena kwa aibu.
23 Watakapowaona watoto wao,watoto niliowajalia mimi mwenyewe,watalitukuza jina langu mimi Mtakatifu wa Yakobo;watakuwa na uchaji kwangu mimi Mungu wa Israeli.
24 Waliopotoka rohoni watapata maarifana wenye kununa watakubali kufunzwa.”