Isaya 27 BHN

1 Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atautwaa upanga wake mkubwa, mkali na imara, na kuliadhibu dude Lewiyathani joka lirukalo na danganyifu; Mwenyezi-Mungu ataliua joka liishilo baharini.

2 Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atasema hivi:“Imbeni utenzi wa shamba langu zuri la mizabibu!

3 Mimi, Mwenyezi-Mungu, ni mkulima wake;nalimwagilia maji kila wakati,ninalilinda usiku na mchana,lisije likaharibiwa na mtu yeyote.

4 Silikasirikii tena shamba hili;kama miiba na mbigili ingelilivamia,mimi ningepambana nayo na kuichoma moto.

5 Maadui za watu wangu wakitaka ulinzi wangu,basi, na wafanye amani nami;naam, wafanye amani nami.”

6 Itakuja siku wazawa wa Yakobo watashika mizizi;naam, watu wa Israeli watachanua na kuchipua,na kuijaza dunia yote kwa matunda.

7 Mungu hakuwaadhibu Waisraeli vikalikama alivyowaadhibu maadui wake;Waisraeli waliopotea vitani,ni wachache kuliko wale wa maadui zake.

8 Aliwaadhibu watu wake kwa kuwapeleka uhamishoni.Wakati wa upepo mkali wa mashariki,aliwaondoa kwa kipigo kikali.

9 Hivi ndivyo uovu wa wazawa wa Yakobo utakavyoondolewa,hivi ndivyo dhambi yake itakavyofutwa kabisa:Ataziharibu madhabahu za miungu;mawe yake yatasagwasagwa kama chokaa;Ashera, wala madhabahu za kufukizia ubani hazitabaki.

10 Mji ule wa ngome sasa umekuwa mtupu,umeachwa na kuhamwa kama jangwa,humo ndama wanalisha na kupumzika.

11 Matawi ya miti yamekauka na kuvunjika;kina mama huyaokota wakawashia moto.Watu hawa hawajaelewa kitu,kwa hiyo Mungu, Muumba wao, hatawahurumia,yeye aliyewafanya, hatawafadhili.

12 Siku hiyo, kutoka mto Eufrate hadi mpakani mwa Misri, Mwenyezi-Mungu ataipura nafaka yake, nanyi Waisraeli mtakusanywa mmojammoja.

13 Siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa na watu wote wa Israeli waliopotea nchini Ashuru au waliotawanywa nchini Misri watarudi na kumwabudu Mwenyezi-Mungu juu ya mlima mtakatifu huko Yerusalemu.