1 Bwana Mwenyezi-Mungu amenijaza roho yake,maana Mwenyezi-Mungu ameniweka wakfu,akanituma niwaletee wanaokandamizwa habari njema,niwatibu waliovunjika moyo,niwatangazie mateka kwamba watapata uhuru,na wafungwa kwamba watafunguliwa.
2 Amenituma niutangaze mwaka wake wa neema,na siku ya Mungu wetu ya kulipiza kisasi;niwafariji wote wanaoomboleza;
3 niwape wale wanaoomboleza katika Siyonitaji la maua badala ya majivu,mafuta ya furaha badala ya maombolezo,vazi la sifa badala ya moyo mzito.Nao wataitwa mialoni madhubuti,aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake.
4 Watayajenga upya magofu ya zamani,wataisimika miji iliyoharibiwa hapo kwanza;wataitengeneza miji iliyobomolewa,uharibifu wa vizazi vingi vilivyopita.
5 Wageni watakuwa hapo kuwachungia mifugo yenu;watawalimia na kuwatunzia mizabibu yenu.
6 Nanyi mtaitwa: “Makuhani wa Mwenyezi-Mungu”,Mtaitwa: “Watumishi wake Mungu wetu”.Mtafaidika kwa utajiri wa mataifa,mtatukuka kwa mali zao.
7 Kwa vile mlipata aibu maradufu,watu wakaona kuwa fedheha ni majaliwa yenu,sasa mtapata eneo maradufu kuwa mali yenu,na furaha yenu itadumu milele.
8 “Mimi Mwenyezi-Mungu napenda haki;nachukia unyanganyi na uhalifu.Nitawatuza watu wangu kwa uaminifu,nitafanya nao agano la milele.
9 Wazawa wao watakuwa maarufu kati ya mataifa;watajulikana kuwa maarufu kati ya watu wengine.Kila atakayewaona atakiri kwambawao ni watu aliowabariki Mwenyezi-Mungu.”
10 Nitafurahi sana kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu,nafsi yangu itashangilia kwa sababu ya Mungu wangu.Maana amenivika vazi la wokovu,amenivalisha vazi la uadilifu,kama bwana arusi ajipambavyo kwa shada la maua,kama bibi arusi ajipambavyo kwa johari zake.
11 Hivyo, kama vile ardhi ioteshavyo mimea,na shamba lichipushavyo mbegu zilizopandwa humo,Mwenyezi-Mungu atasababisha uadilifu na sifakuchomoza mbele ya mataifa yote.