1 Ni nani huyu ajaye kutoka Edomu,anayefika kutoka Bosra na mavazi ya madoa mekundu?Ni nani huyo aliyevaa mavazi ya fahari,anatembea kwa nguvu zake kubwa?Ni mimi Mwenyezi-Munguninayetangaza ushindi wangu;nami ni mwenye nguvu ya kuokoa.
2 Lakini mbona nguo yako ni nyekundu,nyekundu kama ya mtu anayekamua zabibu?
3 “Naam, nimekamua zabibu peke yangu,wala hakuna mtu aliyekuja kunisaidia.Nimeyakanyaga mataifa kwa hasira yangu,niliyapondaponda kwa ghadhabu yangu.Nguo zangu zimejaa madoa ya damu yao,imeyachafua kabisa mavazi yangu.
4 Niliamua kuwa siku ya kulipiza kisasi imefika;wakati wa kuwakomboa watu wangu umefika.
5 Nilitazama na hapakuwa na wa kunisaidia;nilishangaa hapakuwa na wa kuniunga mkono.Lakini nilijipatia ushindi kwa mkono wangu,ghadhabu yangu ilinihimiza.
6 Kwa hasira yangu niliwaponda watu,niliwalewesha kwa ghadhabu yangu;damu yao niliimwaga chini ardhini.”
7 Nitasimulia fadhili za Mwenyezi-Mungu;nitataja matendo yake yote yastahiliyo sifa,kwa sababu ya yote aliyotutendea,wema wake mkuu aliowapa Waisraeli kwa huruma yake,kadiri ya wingi wa fadhili zake.
8 Maana alisema juu yao:“Hakika, hawa ni watu wangu;watoto wangu ambao hawatanidanganya.”Basi yeye akawa Mwokozi wao.
9 Katika taabu zao zote,hakumtuma mjumbe mwingine kuwasaidia,ila yeye mwenyewe alikuja kuwaokoa.kwa upendo na huruma yake aliwakomboa.Aliwabeba na kuwachukua tangu zamani.
10 Lakini wao walikuwa wakaidi,wakaihuzunisha roho yake takatifu.Basi, Mungu akageuka, akawa adui yao;yeye mwenyewe akapigana nao.
11 Ndipo walipokumbuka siku za zamani,wakati wa Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.Wakauliza, “Yuko wapi sasa Mwenyezi-Mungu,aliyewaokoa wachungaji wa kundi lake baharini?Yuko wapi yule aliyeiweka roho yake takatifu kati yao,
12 ambaye kwa mkono wake wenye nguvualifanya maajabu kwa njia ya Mose,akapasua bahari na kuwaongoza watu wake,na kujipatia jina la milele?
13 Aliwaongoza katikati ya vilindi vya bahari,wakapita humo kama farasi bila kujikwaa.
14 Kama ng'ombe wapelekwavyo malishoni bondeni,ndivyo roho ya Mungu ilivyowapumzisha watu wake.Ndivyo ee Mungu ulivyowaongoza watu wako,nawe ukajipatia jina tukufu.”
15 Ututazame kutoka mbinguni ee Mungu, uone,utuangalie kutoka makao yako matakatifu na matukufu.Iko wapi bidii yako kwa ajili yetu na nguvu yako?Usiache kutuonesha upendo wako.
16 Maana wewe ndiwe Baba yetu;Abrahamu, mzee wetu, hatujali,naye Israeli hatutambui;lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ni Baba yetu.Wewe umeitwa tangu kale: “Mkombozi wetu.”
17 Ee Mwenyezi-Mungu, mbona unatukosesha njia zako?Mbona unatufanya kuwa wakaidi hata tusikuogope?Rudi ee Mungu kwa ajili ya watumishi wako,makabila ambayo daima yalikuwa mali yako.
18 Kwa kitambo tu sisi watakatifu wako tulimiliki nchi,lakini maadui zetu wakaja wakaharibu maskani yako.
19 Tumekuwa kama watu ambao hujawatawala kamwe,kama watu ambao hawakujulikana kwa jina lako.