1 Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu,fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka!Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba;na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia!
2 Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu,ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali,kama tufani ya mafuriko makubwa;kwa mkono wake atawatupa chini ardhini.
3 Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimuyatakanyagwakanyagwa ardhini,
4 fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka;fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubaitakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi;mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja.
5 Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu,kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai.
6 Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki,nao walinzi wa mji atawapa nguvu.
7 Lakini wako wengine waliolewa divaina kuyumbayumba kwa sababu ya pombe;naam, makuhani na manabii wamelewa mvinyo,wamevurugika kwa divai.Wanayumbayumba kwa pombe kali;maono yao yamepotoka,wanapepesuka katika kutoa hukumu.
8 Meza zote zimetapakaa matapishi,hakuna mahali popote palipo safi.
9 Wao wananidhihaki na kuuliza:“Huyu nabii ataka kumfundisha nani?Je, anadhani atatueleza sisi ujumbe wake?Je, sisi ni watoto wachangawalioachishwa kunyonya juzijuzi?
10 Anatufundisha kama watoto wadogo:Sheria baada ya sheria,mstari baada ya mstari;mara hiki, mara kile!”
11 Haya basi!Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawakwa njia ya watu wa lugha tofautiwanaoongea lugha ngeni.
12 Hata hivyo yeye alikuwa amewaahidi:“Nitawaonesheni pumziko,nitawapeni pumziko enyi mliochoka.Hapa ni mahali pa pumziko.”Lakini wao hawakutaka kunisikiliza.
13 Kwa hiyo kwao neno la Mwenyezi-Mungu litakuwa tu:Sheria sheria, mstari mstari;mara hiki, mara kile!Nao watalazimika kukimbialakini wataanguka nyuma;watavunjika, watanaswa na kutekwa.
14 Basi, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu,enyi wenye madharau mnaotawala watu wa Yerusalemu,
15 “Nyinyi mnajidai mmefanya mkataba na kifo,mmefanya mapatano na Kuzimu!Nyinyi mwasema eti balaa lijapo halitawapata,kwa sababu mmefanya uongo kuwa tegemeo lenu,na udanganyifu kuwa kinga yenu!”
16 Basi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu:“Tazama! Naweka mjini Siyoni jiwe la msingi,jiwe ambalo limethibitika.Jiwe la pembeni, la thamani,jiwe ambalo ni la msingi thabiti;jiwe lililo na maandishi haya:‘Anayeamini hatatishika.’
17 Nitatumia haki kama kipimo changu,nitatumia uadilifu kupimia.”Mvua ya mawe itaufagilia mbali uongo mnaoutegemea,na mafuriko yataharibu kinga yenu.
18 Hapo mkataba wenu na kifo utabatilishwa,na mapatano yenu na Kuzimu yatafutwa.Janga lile kuu litakapokujalitawaangusheni chini.
19 Kila litakapopitia kwenu litawakumba;nalo litapita kila asubuhi, mchana na usiku.Kusikia ujumbe huu tu kutakuwa kitisho.
20 Kwenu itakuwa kama ajinyoshaye juu ya kitanda kifupi mno,au kujifunika kwa blanketi lililo dogo mno!
21 Maana Mwenyezi-Mungu atainuka kama kule mlimani Perazimu;atawaka hasira kama kule bondeni Gibeoni.Atatekeleza mpango wake wa ajabu;atatenda kazi yake ya kustaajabisha.
22 Basi, nyinyi msiwe na madharauvifungo vyenu visije vikakazwa zaidi.Maana nimesikia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshiameazimia kuiangamiza nchi yote.
23 Tegeni sikio msikilize ninayowaambieni;sikilizeni kwa makini hotuba yangu.
24 Je, alimaye ili kupanda hulima tu?Je, huendelea kulima na kusawazisha shamba lake?
25 La! Akisha lisawazisha shamba lake,hupanda mbegu za bizari na jira,akapanda ngano na shayiri katika safu,na mipakani mwa shamba mimea mingineyo.
26 Mtu huyo huwa anajua la kufanya,kwa sababu Mungu wake humfundisha.
27 Bizari haipurwi kwa mtarimbowala jira kwa gari la ng'ombe!Ila bizari hupurwa kwa kijitina jira kwa fimbo.
28 Mkulima apurapo ngano yake,haendelei kuipura mpaka kuvunja punje zake.Anajua jinsi ya kuipura kwa gurudumu,bila kuziharibu punje za ngano.
29 Ujuzi huu nao watoka kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.Mipango yake Mungu ni ya ajabu,hekima yake ni kamilifu kabisa.