1 Kauli ya Mungu dhidi ya Bonde la Maono.Kuna nini ee Yerusalemu?Mbona watu wote mmepanda juu ya nyumba?
2 Kwa nini mnapiga kelele za shangwe,na mji wote umechangamka na kujaa vigelegele?Watu wenu waliokufa hawakuuawa vitani,wala hawakuuawa katika mapigano.
3 Maofisa wenu wote walikimbia,wakakamatwa hata kabla ya kufyatua mshale mmoja.Watu wako wote waliopatikana walitekwa,ingawa walikuwa wamekimbilia mbali.
4 Ndiyo maana nawaambieni:Msijali chochote juu yanguniacheni nilie machozi ya uchungu.Msijisumbue kunifarijikwa ajili ya balaa walilopata watu wangu.
5 Maana leo Mwenyezi-Mungu wa majeshiametuletea mchafuko:Kushindwa na wasiwasi katika Bonde la Maono.Kuta za mji zimebomolewa,mayowe ya wakazi wake yasikika mpaka milimani.
6 Majeshi ya Elamu, pinde na mishale mikononi,walikuja wamepanda farasi na magari ya vita;nalo jeshi la Kiri lilitayarisha ngao zake.
7 Mabonde yako mazuri ewe Yerusalemu,yalijaa magari ya vita na farasi;wapandafarasi walijipanga tayari langoni mwako.
8 Ulinzi wote wa Yuda uliporomoka.Siku hiyo mlikwenda kutafuta silaha zilizokuwa zimehifadhiwa katika Nyumba ya Msitu,
9 mkaona kwamba nyufa za kuta za mji wa Daudi ni nyingi, mkajaza maji bwawa la chini.
10 Mlizikagua nyumba za mji wa Yerusalemu, mkabomoa baadhi yake ili kupata mawe ya kuimarisha kuta za mji.
11 Katikati ya kuta hizo mlijijengea birika la kuhifadhia maji yanapotiririka kutoka bwawa la zamani. Lakini hamkumtafuta Mungu aliyepanga mambo haya yote; hamkumjali yeye aliyepanga hayo yote tangu zamani.
12 Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu, wa majeshialiwataka mlie na kuomboleza,mnyoe nywele na kuvaa mavazi ya gunia.
13 Lakini nyinyi mkafurahi na kusherehekea.Mlichinja ng'ombe na kondoo,mkala nyama na kunywa divai.Nyinyi mlisema:“Acha tule na kunywamaana kesho tutakufa.”
14 Mwenyezi-Mungu wa majeshi alinifunulia haya akisema:“Hakika hawatasamehewa uovu huu,watakufa bila kusamehewa.Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.”
15 Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliniambia niende kwa Shebna, msimamizi wa jamaa ya kifalme, nikamwambie hivi:
16 “Una haki gani kuwa huku? Je, una ndugu yeyote hapa, hata ukajichongea kaburi mwambani juu ya mlima?
17 Wewe ni mwenye nguvu, lakini Mwenyezi-Mungu atakutupilia mbali kwa nguvu.
18 Atakubana kabisa na kukuzungushazungusha, kisha atakutupa kama mpira mpaka katika nchi pana. Huko utafia karibu na magari yako ya vita unayojivunia. Wewe ni aibu kwa nyumba ya bwana wako.
19 Mwenyezi-Mungu atakungoa madarakani mwako na kukuporomosha kutoka mahali ulipo.
20 “Siku hiyo, nitamleta mtumishi wangu Eliakimu mwana wa Hilkia.
21 Nitamvisha vazi lako rasmi, nitamfunga mshipi wako na kumpa madaraka yako. Yeye atakuwa baba kwa watu wa Yerusalemu na kwa ukoo wa Yuda.
22 Nitamwekea begani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Akifungua, hakuna atakayeweza kufunga na akifunga, hakuna atakayeweza kufungua.
23 Nitamwimarisha Eliakimu kama kigingi kilichofungiwa mahali salama, naye atapata heshima tukufu katika ukoo wa wazee wake.
24 “Watu wote na jamaa yake, wadogo kwa wakubwa watajitegemeza kwake kama chungu na vikombe vilivyotundikwa kwenye kigingi.
25 Lakini siku moja, kama vile kile kigingi kilichofungwa mahali salama kitalegea kwa uzito, Eliakimu naye atapoteza madaraka yake na jamaa zake wote watabaki bila msaada. Mimi Mwenyezi-Mungu nimenena.”