1 Siku ile watu wataimba wimbo huu katika nchi ya Yuda:Sisi tuna mji imara:Mungu anatulinda kwa kuta na ngome.
2 Fungueni malango ya mji,taifa aminifu liingie;taifa litendalo mambo ya haki.
3 Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti,wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.
4 Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zotekwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele.
5 Amewaporomosha waliokaa pande za juu,mji maarufu ameuangusha mpaka chini,ameutupa mpaka mavumbini.
6 Sasa mji huo unakanyagwakanyagwakwa miguu ya watu maskini na fukara.
7 Njia ya watu wanyofu ni rahisi;ewe Mungu mwadilifu, wasawazisha njia yao.
8 Katika njia ya maamuzi yakotunakungojea ee Mwenyezi-Mungu;kulikumbuka jina lako ndiyo tamaa yetu.
9 Moyo wangu wakutamani usiku kucha,nafsi yangu yakutafuta kwa moyo.Utakapoihukumu dunia,watu wote ulimwenguni watajifunza haki.
10 Lakini waovu hata wakipewa fadhili,hawawezi kujifunza kutenda haki.Hata katika nchi ya wanyofu,wao bado wanatenda maovu,wala hawajali ukuu wako wewe Mwenyezi-Mungu.
11 Ee Mwenyezi-Mungu umeinua mkono kuwaadhibu,lakini maadui zako hawauoni.Waoneshe uwapendavyo watu wako nao wataaibika.Moto wa hasira yako uwateketeze maadui zako!
12 Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umetupatia amani;umefanikisha shughuli zetu zote.
13 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,tulipata kutawaliwa na watu wengine na miungu yao,lakini twakiri wewe pekee kuwa Mungu wetu.
14 Watu hao wamekufa, wala hawataishi tena;wamekuwa mizimu, wala hawatafufuka.Maana wewe umewaadhibu na kuwaangamiza,hakuna atakayeweza kuwakumbuka tena.
15 Umelikuza taifa letu, ee Mwenyezi-Mungu,naam, umelizidisha taifa letu.Umeipanua mipaka yote ya nchi,kwa hiyo wewe watukuka.
16 Ee Mwenyezi-Mungu, walipotaabika walikutafuta,walikuomba msaada ulipowaadhibu.
17 Kama vile mama mjamzito anayejifunguahulia na kugaagaa kwa uchungu,ndivyo tulivyokuwa kwa sababu yako, ee Mwenyezi-Mungu.
18 Sisi tulipata maumivu ya kujifungualakini tukajifungua tu upepo!Hatukupata ushindi wowote kwa ajili ya nchi yetu,hatukuweza kuongeza idadi ya watu katika nchi.
19 Wafu wako wataishi tena,miili yao itafufuka.Wanaolala mavumbini wataamka na kuimba kwa furaha!Mungu atapeleka umande wake wa uhai,nao walio kwa wafu watatoka hai.
20 Njoni watu wangu, ingieni majumbani mwenu,mkajifungie humo ndani.Jificheni kwa muda mfupi,mpaka ifike ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
21 Maana Mwenyezi-Mungu aja kutoka kwake juu,kutoka makao yake huko mbinguni;kuwaadhibu wakazi wa dunia kwa uovu wao.Nayo dunia haitaficha tena wale waliouawa,ila itaufichua umwagaji damu wote.