1 Wakati huo, mfalme Merodak-baladani mwana wa Baladani, mfalme wa Babuloni, aliposikia kwamba Hezekia alikuwa ameugua na sasa amepona, alimtumia ujumbe pamoja na zawadi.
2 Basi, Hezekia aliwakaribisha na kuwaonesha nyumba ya hazina: Fedha, dhahabu, viungo vya kukolezea chakula, mafuta ya thamani, vifaa vyake vyote vya kijeshi na vitu vyote vilivyokuwamo katika bohari zake. Hakuna chochote katika ikulu yake au katika nchi yake ambacho hakuwaonesha.
3 Ndipo nabii Isaya alipokwenda kwa mfalme Hezekia na kumwuliza, “Watu hawa wamesema nini? Na, wamekujia kutoka wapi?” Naye Hezekia akamjibu “Wamenijia kutoka nchi ya mbali, huko Babuloni.”
4 Halafu Isaya akamwuliza, “Wameona nini katika ikulu yako?” Hezekia akamjibu, “Wameona yote yaliyomo katika ikulu yangu. Hakuna chochote katika bohari zangu ambacho sikuwaonesha.”
5 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi:
6 Tazama, siku zinakuja ambapo vyote vilivyomo nyumbani mwako na vitu vyote walivyokusanya wazee wako hadi leo, vitapelekwa mpaka Babuloni. Hakuna kitu chochote kitakachobaki; ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu.
7 Tena baadhi ya watoto wako mwenyewe wa kiume watapelekwa mateka nao watakuwa matowashi katika ikulu ya mfalme wa Babuloni.”
8 Naye Hezekia akamwambia Isaya, “Neno la Mwenyezi-Mungu ulilosema ni sawa.” Alisema hivyo kwani alifikiri, “Kutakuwa na amani na usalama muda wote niishipo.”