1 Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe Mungu wangu;nitakutukuza na kulisifu jina lako,kwa maana umetenda mambo ya ajabu;waitekeleza kwa uaminifu na kwelimipango uliyoipanga tangu zamani.
2 Umeufanya mji ule kuwa rundo la mawe,mji wenye ngome kuwa uharibifu.Majumba ya watu wageni yametoweka,wala hayatajengwa tena upya.
3 Kwa hiyo watu wenye nguvu watakutukuza,miji ya mataifa katili itakuogopa.
4 Maana wewe umekuwa ngome kwa maskini,ngome kwa fukara katika taabu zao.Wewe ni kimbilio wakati wa tufani,kivuli wakati wa joto kali.Kweli pigo la watu wakatili ni kalikama tufani inayopiga ukuta;
5 ni kama joto la jua juu ya nchi kavu.Lakini wewe wakomesha fujo ya wageni.Kama wingu lizimavyo joto la juandivyo ukomeshavyo nyumba za ushindi za wakatili.
6 Juu ya mlima Siyoni, Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawafanyia watu wote karamu ya vinono na divai nzuri, nyama tamu na mafuta, pamoja na divai safi.
7 Katika mlima huuhuu, Mwenyezi-Mungu ataliondoa wingu la huzuni lililowafunika watu wote, kifuniko cha uchungu juu ya mataifa yote.
8 Bwana Mungu atakiangamiza kifo milele! Atayafuta machozi katika nyuso za watu wote na kuwaondolea watu wake aibu duniani kote. Bwana Mwenyezi-Mungu ametamka.
9 Siku ile, watu wote watasema, “Huyu ndiye Mungu wetu! Tumemngojea atuokoe. Huyu ndiye Mwenyezi-Mungu tuliyemtazamia. Njoni tufurahi na kushangilia kwa kuwa ametuokoa.”
10 Mwenyezi-Mungu ataulinda mlima wa Siyoni, lakini watu wa Moabu watakanyagwakanyagwa nchini mwao kama nyasi katika shimo la mbolea.
11 Watainyosha mikono yao kama mtu anayejaribu kuogelea, lakini pamoja na ustadi wao, Mwenyezi-Mungu ataporomosha kiburi chao.
12 Atayabomoa maboma ya miji ya Moabu yenye kuta ndefu na kuyabwaga chini mavumbini.