1 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Nisikilizeni enyi mnaotaka kukombolewa,nyinyi mnaonitafuta mimi Mwenyezi-Mungu.Utazameni mwamba mlimochongwa,chimbo la mawe mlimochimbuliwa.
2 Mkumbukeni Abrahamu babu yenu,na Sara aliyewazaa nyinyi.Abrahamu alikuwa hana mtoto wakati nilipomwita,lakini nilimbariki na kumfanya kuwa na wengi.
3 “Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji mji wa Siyoni,nitaparekebisha mahali pake pote palipoharibika.Nyika zake nitazifanya kama bustani ya Edeni,majangwa yake kama bustani ya Mwenyezi-Mungu.Kwake kutapatikana furaha na shangwe,na nyimbo za shukrani zitasikika humo.
4 “Nisikilizeni enyi watu wangu,nitegeeni sikio enyi taifa langu.Sheria na haki zitatoka kwangu mimi;nazo zitakuwa mwanga wa mataifa.
5 Nitaleta ukombozi hima;wokovu nitakaoleta waanza kutokea.Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa.Wakazi wa nchi za mbali wananingojea,wanaitegemea nguvu yangu.
6 Inueni macho mzitazame mbingu,kisha tazameni dunia huko chini.Mbingu zitatoweka kama moshi,dunia itachakaa kama vazi,na wakazi wake watakufa kama wadudu.Lakini wokovu niuletao wadumu milele;ukombozi wangu kamwe hautakoma.
7 “Nisikilizeni enyi mjuao mambo ya haki,ambao sheria zangu zimo mioyoni mwenu.Msiogope dharau za watu,wala kufadhaishwa na masimango yao.
8 Maana wataliwa na nondo kama vile vazi;viwavi watawala kama walavyo nguo ya sufu.Lakini ukombozi niletao mimi utadumu milele;wokovu wangu hautakuwa na mwisho.”
9 Amka! Amka ee Mwenyezi-Mungu!Jivike nguvu zako utuokoe.Amka kama ulivyofanya hapo zamani,nyakati za vizazi vya hapo kale.Je, si wewe uliyemkatakata Rahabu,ukalitumbua dude hilo la kutisha?
10 Wewe ndiwe uliyeikausha bahari,ndiwe uliyevikausha vilindi vya maji,ukafanya njia katika vilindi vya bahari,ili wale uliowakomboa wavuke humo.
11 Watu wako uliowakomboa, ee Mwenyezi-Mungu, watarudi,watakuja Siyoni wakiimba;watajaa furaha ya milele,watapata furaha na shangwe.Huzuni na maombolezo vitatoweka kabisa.
12 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Mimi, naam mimi, ndimi ninayekufariji.Kwa nini wewe unamwogopa mtu ambaye hufa,binadamu ambaye hutoweka kama nyasi?
13 Wewe umenisahau mimi Mwenyezi-Mungu Muumba wako,niliyezitandaza mbingu,na kuiweka misingi ya dunia!Wewe waendelea kuogopa siku zote,kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu wako,kwamba yuko tayari kukuangamiza!Lakini hasira yake itafika wapi?
14 Wanaodhulumiwa watafunguliwa hima,hawatakufa na kushuka shimoni,wala hawatatindikiwa chakula.
15 Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako;nivurugaye bahari, mawimbi yake yakanguruma;Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina langu!
16 Nimeyaweka maneno yangu mdomoni mwako;nimekuficha katika kivuli cha mkono wangu.Mimi nilizitandaza mbingu,nikaiweka misingi ya dunia.Mimi nawaambieni enyi watu wa Siyoni:‘Nyinyi ni watu wangu.’”
17 Amka ewe Yerusalemu!Amka usimame wima!Mwenyezi-Mungu amekunywesha kikombe cha ghadhabu yake,nawe umeinywa mpaka tone la mwisho,mpaka ukayumbayumba.
18 Kati ya watoto wote uliowazaahakuna yeyote wa kukuongoza.Hakuna hata mmoja wa kukushika mkonokati ya watoto wote uliowalea.
19 Majanga haya mawili yamekupata:Uharibifu na maangamizi; njaa na mauaji.Nani atakayekuonea huruma?Nani atakayekufariji?
20 Watoto wako wamezirai,wamelala pembeni mwa kila barabara,wako kama paa aliyenaswa wavuni.Wamepatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu,wamepatwa na adhabu ya Mungu wako.
21 Basi, sikiliza ewe Yerusalemu unayeteseka;sikiliza wewe uliyelewa, lakini sio kwa divai.
22 Bwana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,awateteaye watu wake, asema hivi:“Nimekuondolea kikombe cha kuyumbisha,hutakunywa tena kikombe cha ghadhabu yangu.
23 Nitawanywesha watesi wako kikombe hichowaliokuambia ulale chini wapite juu yako;wakaufanya mgongo wako kama ardhi,kama barabara yao ya kupitia.”