1 Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Koreshi:“Wewe ni mfalme wangu niliyekuteua;mimi naitegemeza nguvu yakoili uyashinde mataifa mbele yako,na kuzivunja nguvu za wafalme.Mimi nayafungua malango ya mji mbele yako,na hakuna lango litakalofungwa.
2 Mimi nitakutangulia,na kuisawazisha milima mbele yako.Nitaivunjavunja milango ya shaba,na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma.
3 Nitakupa hazina zilizofichwa gizani,na mali iliyo mahali pa siri,upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu,Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako.
4 Kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo,naam, kwa ajili ya mteule wangu Israeli,nimekuita kwa jina lako;nimekupa jina la heshima ingawa wewe hunijui.
5 “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine;hakuna Mungu mwingine ila mimi.Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui,
6 ili watu wote, toka mashariki hadi magharibi,wajue kwamba hakuna Mungu mwingine ila mimi;mimi ni Mwenyezi-Mungu na hakuna mwingine.
7 Mimi hufanya mwanga na kuumba giza;huleta fanaka na kusababisha balaa.Mimi Mwenyezi-Mungu hutenda vitu hivi vyote.
8 Enyi mbingu, nyesheni kutoka huko juu,mawingu na yadondoshe uadilifu;dunia na ifunuke, ichipushe wokovu,na kuchanusha uadilifu pia!Mimi, Mwenyezi-Mungu nimefanya hayo.”
9 Ole wake mtu ashindanaye na Muumba wake,mtu aliye chombo cha udongokushindana na mfinyanzi wake!Je, udongo humwuliza anayeufinyanga:“Unatengeneza nini hapa?”Au kumwambia, “Kazi yako si kamili!”
10 Ole wake mtoto amwambiaye baba yake,“Kwa nini umenizaa?”Au amwambiaye mama yake,“Ya nini umenileta duniani?”
11 Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli,Mungu, Muumba wa Israeli asema:“Je, mwathubutu kuniuliza juu ya watoto wangu,au kuniamuru juu ya kazi zangu mwenyewe?
12 Ni mimi niliyeifanya dunia,na kuumba binadamu aishiye humo.Mikono yangu ndiyo iliyozitandaza mbingu,na jeshi lote la nyota liko kwa amri yangu.
13 Ni mimi niliyemwamuru Koreshi kuchukua hatua,atekeleze matakwa yangu.Nitazifanikisha njia zake zote;ataujenga upya mji wangu Yerusalemu,na kuwapa uhuru watu wangu walio uhamishoni,bila kutaka malipo wala zawadi.”Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema.
14 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Utajiri wa Misri na bidhaa za Kushi,pamoja na za watu wa Seba, majitu marefu,zitakuja kwako mwenyewe wewe taifa la Israeli,zote zitakuwa mali yako.Watu hao watakutumikia wamefungwa minyororo;watakusujudia na kukiri wakisema:‘Kwako kuna Mungu wa kweli,wala hakuna Mungu mwingine ila yeye.’”
15 Kweli wewe ni Mungu uliyefichika,Mungu wa Israeli, Mungu Mwokozi.
16 Watengenezaji sanamu wataaibika na kufadhaika,wote kwa pamoja watavurugika.
17 Lakini taifa la Israeli litaokolewa na Mwenyezi-Mungu,litapata wokovu wa milele.Halitaaibishwa wala kufadhaishwa milele.
18 Mwenyezi-Mungu, Mungu pekee,ndiye aliyeiumba dunia,ndiye aliyeiumba na kuitegemeza.Hakuiumba iwe ghasia na tupu,ila aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.Yeye asema sasa:“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu,wala hakuna mwingine.
19 Mimi sikunena kwa siri,wala katika nchi yenye giza.Mimi sikuwaambia wazawa wa Yakobowanitafute katika ghasia.Mimi Mwenyezi-Mungu husema ukweli,maneno yangu ni ya kuaminika.”
20 Enyi watu wa mataifa mliosalia,kusanyikeni pamoja mje!Nyinyi mmekosa akili:Nyinyi mwabeba sanamu za mitina kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu.
21 Semeni wazi na kutoa hoja zenu;shaurianeni pamoja!Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa?Ni nani aliyetamka mambo haya zamani?Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu?Hakuna Mungu mwingine ila mimi!Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi;hakuna mwingine ila mimi.
22 Nigeukieni mimi mpate kuokolewa,popote mlipo duniani.Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine.
23 Mimi nimeapa kwa nafsi yangu,ninachotamka ni ukweli,neno langu halitarudi nyuma:Kila binadamu atanipigia magoti,kila mtu ataapa uaminifu.
24 “Watasema juu yangu,‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’”Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Munguwatamjia yeye na kuaibishwa.
25 Lakini wazawa wa Israeliwatapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi.