1 Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Ole wao watoto wanaoniasi,wanaotekeleza mipango yao na si mipango yangu,wanaofanya mikataba kinyume cha matakwa yangu!Naam, wanarundika dhambi juu ya dhambi.
2 Bila kunitaka shauri, wanafunga safari kwenda Misri,kukimbilia usalama katika ulinzi wa Farao,kupata mahali pa usalama nchini Misri.
3 Lakini ulinzi wa Farao utakuwa aibu yenu,na usalama nchini Misri utakuwa fedheha yenu.
4 Maana ingawa maofisa wao wamefika Soani,na wajumbe wao mpaka Hanesi,
5 wote wataaibishwa na hao wasioweza kuwasaidia,watu ambao hawawezi kuwapa msaada au faida,ila tu kuwapa aibu na fedheha.”
6 Kauli ya Mungu juu ya wanyama wa pande za Negebu:“Wajumbe wanapita katika nchi ya taabu na shida,yenye simba, nyoka wa sumu na majoka.Wamewabebesha wanyama wao mali zao,kuwapelekea watu wasioweza kuwafaa kitu.
7 Maana msaada wa Misri ni bure, haufai kitu;kwa hiyo nimeipanga Misri jina:‘Joka lisilo na nguvu!’”
8 Mungu aliniambia:“Sasa chukua kibao cha kuandikia,uandike jambo hili mbele yao,liwe ushahidi wa milele:
9 Watu hawa ni waasi, watoto wasioaminika;watu wasiopenda kusikia mafunzo ya Mwenyezi-Mungu.
10 Huwaambia waonaji: ‘Msione maono’,na manabii: ‘Msitutangazie ukweli,bali tuambieni mambo ya kupendeza,toeni unabii wa mambo ya udanganyifu tu.
11 Geukeni na kuiacha njia ya ukweli;msituambie tena juu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli.’”
12 Kwa hiyo Mungu, Mtakatifu wa Israeli asema:“Nyinyi mmeukataa ujumbe wangu;mkapania kufanya dhuluma na udanganyifu.
13 Basi, dhambi hii itawaleteeni maangamizikama ufa mkubwa katika ukuta mrefu;utabomoka mara na kuanguka chini ghafla.
14 Kuporomoka kwa ukuta huo,ni kama kupasuka kwa chunguambacho kimepasuliwa vibaya sana,bila kusalia kigae cha kuchukulia moto mekoni,au kuchotea maji kisimani.”
15 Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema:“Mkinirudia na kutulia mtaokolewa;kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.”Lakini nyinyi hamkutaka.
16 Badala yake mlisema,“La! Sisi tutakimbia na farasi wenye mbio.”Sawa, mtakimbia na farasi wenye mbio,lakini farasi wa maadui zenu wana mbio zaidi.
17 Watu wenu elfu moja watamkimbia askari mmoja adui;na askari watano maadui watawakimbizeni nyote.Mwishowe, watakaosaliawatakuwa kama mlingoti wa bendera mlimani,kama alama iliyo juu ya kilima.
18 Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu anangoja awafadhili,atainuka na kuwaonea huruma.Maana, Mwenyezi-Mungu ni Mungu atendaye haki.Heri wote wale wanaomtumainia.
19 Enyi watu wa Siyoni, enyi watu wa Yerusalemu, hakika nyinyi hamtaomboleza tena. Kweli Mungu atawahurumia; mara tu atakaposikia kilio chenu atawaitikeni.
20 Ingawa Bwana atawalisha taabu na kuwanywesha dhiki, yeye ndiye Mwalimu wenu na hatajificha tena; nanyi mtamwona kwa macho yenu wenyewe.
21 Mkienda kulia au kushoto, mtasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Njia ni hii; ifuateni.”
22 Mtavifanya haramu vinyago vyenu vya miungu vilivyopakwa fedha na sanamu zenu zilizopakwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitu najisi, mkisema, “Poteleeni mbali!”
23 Mtakapopanda mbegu zenu, Mwenyezi-Mungu atanyesha mvua kwa wakati wake, nazo zitakua na kuwapa mavuno mengi. Mifugo yenu nayo itapata malisho kwa wingi.
24 Mafahali na punda wenu wa kulimia watapata malisho yaliyochambuliwa vizuri na kutiwa chumvi.
25 Wakati utakapofika ambapo maadui watauawa na ngome zao kubomolewa, vijito vya maji vitatiririka kutoka kila mlima na kilima.
26 Tena mwezi utawaka kama jua, nao mwanga wa jua utakuwa mara saba ya mwanga wake wa kawaida, kana kwamba mwanga wa siku saba umeangaza katika siku moja. Mambo haya yote yatatukia wakati Mwenyezi-Mungu atakapoyafunga na kuyaponya majeraha aliyowaletea watu wake.
27 Tazameni, Mwenyezi-Mungu mwenyewe anakuja toka mbali!Amewaka hasira na moshi wafuka;midomo yake yaonesha ghadhabu yake,maneno anayosema ni kama moto uteketezao.
28 Pumzi yake ni kama mafuriko ya mtoambao maji yake yanafika hadi shingoni.Anakuja kuyachekecha mataifa kwa chekecheke ya maangamizi,kuwafunga lijamu na kuwapeleka wasikotaka.
29 Lakini nyinyi watu wa Yerusalemu mtaimba kwa furaha kama mfanyavyo wakati wa mkesha wa sikukuu. Mtajaa furaha kama watu wanaotembea kwa mdundo wa muziki wa filimbi kwenda mlimani kwa Mwenyezi-Mungu, Mwamba wa Israeli.
30 Mwenyezi-Mungu atawafanya watu wote waisikie sauti yake tukufu na pigo la nguvu yake lionekane kwa hasira nyingi. Kutakuwa na ndimi za moto mkali, ngurumo, dhoruba na mvua ya mawe.
31 Waashuru watajaa hofu watakaposikia sauti ya Mwenyezi-Mungu wakati atakapowachapa na fimbo yake.
32 Kila pigo la adhabu ya Mwenyezi-Mungu juu ya Waashuru litaandamana na mdundo wa ngoma na zeze. Yeye mwenyewe binafsi atapigana na Waashuru.
33 Naam, mahali pa kumteketeza mfalme wa Ashuru pamekwisha tayarishwa muda mrefu uliopita. Mahali penyewe ni shimo kubwa na pana. Moto upo na kuni kwa wingi. Mwenyezi-Mungu ataupulizia pumzi yake kama kijito cha madini ya kiberiti na kuuwasha.