1 Karibieni mkasikilize enyi mataifa,tegeni sikio enyi watu.Sikiliza ee dunia na vyote vilivyomo,ulimwengu na vyote vitokavyo humo!
2 Mwenyezi-Mungu ameyakasirikia mataifa yote,ameghadhabika dhidi ya majeshi yao yote.Ameyapangia mwisho wao,ameyatoa yaangamizwe.
3 Maiti zao zitatupwa nje;harufu ya maiti zao itasambaa;milima itatiririka damu yao.
4 Jeshi lote la angani litaharibika,anga zitakunjamana kama karatasi.Jeshi lake lote litanyauka,kama majani ya mzabibu yanyaukavyo,naam, kama tunda la mtini linyaukavyo.
5 Upanga wa Mungu uko tayari juu mbinguni.Tazama, washuka kuwaadhibu Waedomu,watu ambao ameamua kuwaangamiza.
6 Upanga utalowa damu na kutapakaa mafuta,kama kwa damu ya kondoo na mbuzi,na mafuta ya figo za kondoo dume.Maana Mwenyezi-Mungu atatoa kafara huko Bosra,kutakuwa na mauaji makubwa nchini Edomu.
7 Nyati wataangamia pamoja nao,ndama kadhalika na mafahali.Nchi italoweshwa damu,udongo utarutubika kwa mafuta yao.
8 Maana Mwenyezi-Mungu anayo siku ya kisasi;mwaka wa kulipiza maadui wa Siyoni.
9 Vijito vya Edomu vitatiririka lami,udongo wake utakuwa madini ya kiberiti;ardhi yake itakuwa lami iwakayo.
10 Itawaka usiku na mchana bila kuzimika,moshi wake utafuka juu milele.Nchi itakuwa jangwa siku zote,hakuna atakayepitia huko milele.
11 Itakuwa makao ya kozi na nungunungu,bundi na kunguru wataishi humo.Mwenyezi-Mungu atawaletea ghasia,na timazi la fujo kwa wakuu wake.
12 Nchi itaitwa “Nchi bila Mfalme;”wakuu wake wote wametoweka.
13 Miiba itaota katika ngome zake,viwavi na michongoma mabomani mwao.Itakuwa makao ya mbwamwitu, maskani yao mbuni.
14 Pakamwitu na fisi watakuwa humo,majini yataitana humo;kwao usiku utakuwa mwanga,na humo watapata mahali pa kupumzikia.
15 Humo bundi watataga mayai na kuyaatamia,wataangua vifaranga na kuviweka kivulini mwao.Humo vipanga watakutania,kila mmoja na mwenzake.
16 Someni katika kitabu cha Mwenyezi-Mungu:“Hakuna hata kiumbe kimoja kitakachokosekana,kila kimoja kitakuwako na mwenzake.”Maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hivyo,roho yake itawakusanya hao wote.
17 Mwenyezi-Mungu amepanga sehemu ya kila mmoja wao,ametumia kamba kuwapimia nchi hiyo;wataimiliki milele na milele,wataishi humo kizazi hata kizazi.