1 Bwana Mwenyezi-Mungu amenijaza roho yake,maana Mwenyezi-Mungu ameniweka wakfu,akanituma niwaletee wanaokandamizwa habari njema,niwatibu waliovunjika moyo,niwatangazie mateka kwamba watapata uhuru,na wafungwa kwamba watafunguliwa.
2 Amenituma niutangaze mwaka wake wa neema,na siku ya Mungu wetu ya kulipiza kisasi;niwafariji wote wanaoomboleza;
3 niwape wale wanaoomboleza katika Siyonitaji la maua badala ya majivu,mafuta ya furaha badala ya maombolezo,vazi la sifa badala ya moyo mzito.Nao wataitwa mialoni madhubuti,aliyopanda Mwenyezi-Mungu kuonesha utukufu wake.
4 Watayajenga upya magofu ya zamani,wataisimika miji iliyoharibiwa hapo kwanza;wataitengeneza miji iliyobomolewa,uharibifu wa vizazi vingi vilivyopita.
5 Wageni watakuwa hapo kuwachungia mifugo yenu;watawalimia na kuwatunzia mizabibu yenu.