9 Katika mlima mtakatifu wa Munguhakutakuwa na madhara wala uharibifu.Maana kumjua Mwenyezi-Mungu kutaenea pote nchini,kama vile maji yajaavyo baharini.
10 Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka.
11 Siku hiyo, Bwana ataunyosha mkono wake tena kuwarejesha watu wake waliosalia huko Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi na sehemu za pwani.
12 Naye atatweka bendera kuwaashiria mataifa,kuwakusanya Waisraeli waliodharauliwa,kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa,na kuwarudisha toka pembe nne za dunia.
13 Wivu wa Efraimu juu ya Yuda utakoma,hakutakuwa tena na uadui kati ya Yuda na Efraimu.
14 Wote pamoja watawavamia Wafilisti walio magharibi,pamoja watawapora watu wakaao mashariki.Watawashinda Waedomu na Wamoabu,nao Waamoni watawatii.
15 Mwenyezi-Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Shamu,kwa pumzi yake ichomayo atakausha mto Eufrate,nao utagawanyika katika vijito saba,watu wavuke humo miguu mikavu.