2 Basi, nikajipatia mashahidi wawili waaminifu ambao wangenishuhudia: Kuhani Uria na Zekaria, mwana wa Yeberekia.
3 Nililala na mke wangu ambaye pia ni nabii, akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Mpe mtoto huyo jina ‘Teka-haraka-pokonya-upesi.’
4 Maana kabla mtoto huyu hajafikia umri wa kuweza kutamka: ‘Baba’ au ‘Mama,’ utajiri wa Damasko na nyara walizoteka huko Samaria zitapelekwa kwa mfalme wa Ashuru.”
5 Mwenyezi-Mungu aliongea nami tena, akaniambia,
6 “Kwa kuwa watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yatiririkayo polepole, wakafa moyo mbele ya mfalme Resini na mfalme Peka mwana wa Remalia,
7 basi, mimi Bwana nitawaletea mafuriko makuu ya maji ya mto Eufrate yaani mfalme wa Ashuru na nguvu zake zote; yatafurika na kupita kingo zake.
8 Utaingia nchini Yuda kwa nguvu na kufurika na kupanda mpaka shingoni; utaenea juu ya nchi yako yote, ee Emanueli!”