1 Msifikiri mkono wa Mungu ni mfupi,hata asiweze kuwaokoeni;au masikio yake yamezibika,hata asiweze kuwasikieni.
2 Dhambi zenu ndizo zinazowatenga na Mungu wenu,dhambi zenu zimemfanya ajifiche mbali nanyihata asiweze kuwasikieni.
3 Maana mikono yenu imetiwa najisi kwa mauaji,na vidole vyenu kwa matendo maovu.Midomo yenu imesema uongo,na ndimi zenu husema uovu.
4 Hakuna atoaye madai yake kwa haki,wala anayeshtaki kwa uaminifu.Mnategemea hoja batili;mnasema uongo.Mnatunga hila na kuzaa uovu.
5 Mnaangua mayai ya joka lenye sumu,mnafuma utando wa buibui.Anayekula mayai yenu hufa,na yakipasuliwa nyoka hutokea.
6 Utando wenu haufai kwa mavazi,watu hawawezi kujifunikia mnachofuma.Kazi zenu ni kazi za uovu,matendo yenu yote ni ukatili mtupu.