13 Tumekuasi na kukukana ee Mwenyezi-Mungu,tumekataa kukufuata ewe Mungu wetu.Udhalimu na uasi ndivyo tunavyopania,mioyoni mwetu twatunga na kutoa maneno ya uongo.
14 Haki imewekwa kando,uadilifu uko mbali;ukweli unakanyagwa mahakamani,uaminifu haudiriki kuingia humo.
15 Ukweli umekosekana,naye anayeacha uovu hunyanyaswa.Mungu aliona mambo hayo, akachukizwa,alichukizwa kwamba hakuna haki.
16 Aliona kwamba hakuna mtu aliyejali,akashangaa kwamba hakuna aliyeingilia kati.Basi akaamua kunyosha mkono wake mwenyewe,uadilifu wake ukamhimiza.
17 Alivaa uadilifu kama vazi la kujikinga kifuani,na wokovu kama kofia ya chuma kichwani.Atajivika kisasi kama vazi,na kujifunika wivu kama joho.
18 Atawaadhibu maadui kadiri ya matendo yao,naam, ghadhabu yake na kisasi vitawapata maadui zake;atawaadhibu hata wakazi wa nchi za mbali.
19 Toka magharibi hadi mashariki,kila mtu atamcha Mwenyezi-Munguna kutambua utukufu wake.Maana atakuja kama mto uendao kasi,mto unaosukumwa kwa upepo wa Mwenyezi-Mungu.