1 Unilinde ee Mungu;maana kwako nakimbilia usalama.
2 Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu;sina jema lolote ila wewe.”
3 Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini,kukaa nao ndiyo furaha yangu.
4 Lakini wanaoabudu miungu mingine,watapata mateso mengi.Tambiko ya damu sitaitolea kamwe,na majina ya miungu hiyo sitayataja.
5 Wewe ee Mwenyezi-Mungu ndiwe riziki yangu kuu,majaliwa yangu yamo mikononi mwako.
6 Umenipimia sehemu nzuri sana;naam, urithi wangu ni wa kupendeza.
7 Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza,usiku dhamiri yangu yanionya.
8 Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima;yuko pamoja nami, wala sitatikisika.
9 Kwa hiyo nitafurahi kwa moyo wote na kushangilia,nami nitakaa salama salimini.
10 Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu,hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza.
11 Wanionesha njia ya kufikia uhai;kuwako kwako kwanijaza furaha kamili,katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.