1 Heri mtu anayewajali maskini;Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida.
2 Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai,naye atafanikiwa katika nchi;Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake.
3 Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa,atamponya maradhi yake yote.
4 Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu,unihurumie maana nimekukosea wewe.”
5 Madui zangu husema vibaya juu yangu:“Atakufa lini na jina lake litoweke!”
6 Wanitembeleapo husema maneno matupu;wanakusanya mabaya juu yangu,na wafikapo nje huwatangazia wengine.
7 Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu;wananiwazia mabaya ya kunidhuru.
8 Husema: “Maradhi haya yatamuua;hatatoka tena kitandani mwake!”
9 Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini,rafiki ambaye alishiriki chakula changu,amegeuka kunishambulia!
10 Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma!Unipe nafuu, nami nitawalipiza.
11 Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami,maadui zangu wasipopata fahari juu yangu.
12 Wewe umenitegemeza kwani natenda mema;waniweka mbele yako milele.
13 Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,tangu milele na hata milele!Amina! Amina!