1 Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2 Mishale yako imenichoma;mkono wako umenigandamiza.
3 Hamna mahali nafuu mwilini mwangu,kwa sababu umenikasirikia;hamna penye afya hata mifupani mwangu,kwa sababu ya dhambi yangu.
4 Nimefunikwa kabisa na dhambi zangu,zinanilemea kama mzigo mzito mno kwangu.
5 Madonda yangu yameoza na kunuka,na hayo ni matokeo ya ujinga wangu.
6 Nimepindika mpaka chini na kupondeka;mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7 Viungo vyangu vimeshambuliwa na homa;mwilini mwangu hamna nafuu yoyote.
8 Nimelegea na kupondekapondeka;nasononeka kwa kusongwa moyoni.
9 Ee Bwana, wewe wajua tazamio langu lote;kwako hakikufichika kilio changu.
10 Moyo wanidunda, nguvu zimeniishia;hata macho yangu nayo yamekwisha fifia.
11 Rafiki na wenzangu wanaepa kuona mateso yangu,na jamaa zangu wanakaa mbali nami.
12 Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao;wanaonitakia niumie wanatishia kuniangamiza.Mchana kutwa wanafanya mipango dhidi yangu.
13 Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii;nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu.
14 Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia,kama mtu asiye na chochote cha kujitetea.
15 Lakini ninakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu;wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, ndiwe utakayenijibu.
16 Nakuomba tu maadui wasinisimange,wasione fahari juu ya kuanguka kwangu.
17 Karibu sana nitaanguka;nakabiliwa na maumivu ya daima.
18 Naungama uovu wangu;dhambi zangu zanisikitisha.
19 Maadui zangu hawajambo, wana nguvu;ni wengi mno hao wanaonichukia bure.
20 Hao wanaonilipa maovu kwa wema wangu,wananipinga kwa sababu natenda mema.
21 Usinitupe, ee Mwenyezi-Mungu;ee Mungu wangu, usikae mbali nami.
22 Uje haraka kunisaidia;ewe Mwenyezi-Mungu, uliye wokovu wangu.