1 Ee Mwenyezi-Mungu, mbona wasimama mbali?Kwa nini wajificha wakati tumo taabuni?
2 Kwa kiburi waovu wanawatesa maskini;njama zao ziwanase wao wenyewe.
3 Mwovu hujisifia tamaa zake mbaya,mtu wa tamaa hulaani na kumkataa Mwenyezi-Mungu.
4 Katika majivuno yake husema: “Mungu hatagundua.”Mawazo yake yote ni: “Hakuna Mungu.”
5 Njia za mwovu hufanikiwa daima;kwake hukumu zako ziko mbali na mawazo yake,na huwadharau maadui zake wote.
6 Huwaza moyoni: “Sitakuwa na wasiwasi;sitapatwa na dhiki maishani.”
7 Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma;mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu.
8 Hujificha vijijini huku anaotea,amuue kwa siri mtu asiye na hatia.Yuko macho kumvizia mnyonge;
9 huotea mafichoni mwake kama simba.Huvizia apate kuwakamata maskini;huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua.
10 Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini;huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu.
11 Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau;ameficha uso wake, haoni kitu!”
12 Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwaadhibu;usiwasahau wanaodhulumiwa.
13 Ee Mungu, kwa nini mwovu anakudharau,na kusema ati hutamfanya awajibike?
14 Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida;nawe daima uko tayari kuwasaidia.Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu,wewe umekuwa daima msaada wa yatima.
15 Uzivunje nguvu za mtu mwovu;ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena.
16 Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele!Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake.
17 Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge;wampa moyo na kumtegea sikio.
18 Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa,binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu.