1 Ee Mwenyezi-Mungu usikie kisa changu cha haki,usikilize kilio changu,uitegee sikio sala yangu isiyo na hila.
2 Haki yangu na ije kutoka kwako,kwani wewe wajua jambo lililo la haki.
3 Wewe wajua kabisa moyo wangu;umenijia usiku, kunichunguza,umenitia katika jaribio;hukuona uovu ndani yangu,sikutamka kitu kisichofaa.
4 Kuhusu matendo watendayo watu;mimi nimeitii amri yako,nimeepa njia ya wadhalimu.
5 Nimefuata daima njia yako;wala sijateleza kamwe.
6 Nakuita, ee Mungu, kwani wewe wanijibu;unitegee sikio, uyasikie maneno yangu.
7 Onesha fadhili zako za ajabu,uwaokoe kutoka kwa adui zao,wale wanaokimbilia usalama kwako.
8 Unilinde kama mboni ya jicho;unifiche kivulini mwa mabawa yako,
9 mbali na mashambulio ya waovu,mbali na maadui zangu hatari wanaonizunguka.
10 Hao hawana huruma yoyote moyoni;wamejaa maneno ya kujigamba.
11 Wananifuatia na kunizunguka;wananivizia waniangushe chini.
12 Wako tayari kunirarua kama simba:Kama mwanasimba aviziavyo mawindo.
13 Inuka, ee Mwenyezi-Mungu,uwakabili na kuwaporomosha.Kwa upanga uiokoe nafsi yangu kutoka kwa waovu.
14 Kwa mkono wako, ee Mwenyezi-Mungu,uniokoe mikononi mwa watu hao,watu ambao riziki yao ni dunia hii tu. Uwajaze adhabu uliyowawekea,wapate ya kuwatosha na watoto wao,wawaachie hata na wajukuu zao.
15 Lakini mimi nitauona uso wako, kwani ni mwadilifu;niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.