1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?Mbona uko mbali sana kunisaidia,mbali na maneno ya kilio changu?
2 Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu;napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati.
3 Hata hivyo, wewe ni mtakatifu;wewe watawala na kusifiwa na Waisraeli.
4 Wazee wetu walikutegemea;walikutegemea, nawe ukawaokoa.
5 Walikulilia wewe, wakaokolewa;walikutegemea, nao hawakuaibika.
6 Lakini mimi ni mdudu tu, wala si mtu;nimepuuzwa na kudharauliwa na watu.
7 Wote wanionao hunidhihaki;hunifyonya na kutikisa vichwa vyao.
8 Husema: “Alimtegemea Mwenyezi-Mungu,basi, Mungu na amkomboe!Kama Mungu anapendezwa naye,basi, na amwokoe!”
9 Lakini ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,uliniweka salama kifuani pa mama yangu.
10 Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu.Tangu nilipozaliwa wewe umekuwa Mungu wangu.
11 Usikae mbali nami, kwani taabu imekaribia;wala hakuna wa kunisaidia.
12 Maadui wengi wanizunguka kama fahali;wamenisonga kama fahali wakali wa Bashani!
13 Wanafunua vinywa vyao kama simba,tayari kushambulia na kurarua.
14 Nimekwisha kama maji yaliyomwagika;mifupa yangu yote imeteguka;moyo wangu ni kama nta,unayeyuka ndani mwangu.
15 Koo langu limekauka kama kigae;ulimi wangu wanata kinywani mwangu.Umeniacha kwenye mavumbi ya kifo.
16 Genge la waovu limenizunguka;wananizingira kama kundi la mbwa;wamenitoboa mikono na miguu.
17 Nimebaki mifupa mitupu;maadui zangu waniangalia na kunisimanga.
18 Wanagawana nguo zangu,na kulipigia kura vazi langu.
19 Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu, usikae mbali nami;ewe msaada wangu, uje haraka kunisaidia.
20 Iokoe nafsi yangu mbali na upanga,yaokoe maisha yangu makuchani mwa mbwa hao!
21 Uniokoe kinywani mwa simba;iokoe nafsi yangu dhaifu toka pembe za nyati hao.
22 Nitawasimulia ndugu zangu matendo yako;nitakusifu kati ya kusanyiko lao:
23 Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, msifuni!Mtukuzeni enyi wazawa wote wa Yakobo!Mcheni Mungu enyi wazawa wote wa Israeli!
24 Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge;wala hajifichi mbali naye,ila humsikia anapomwomba msaada.
25 Kwa sababu yako ninakusifukatika kusanyiko kubwa la watu;nitatimiza ahadi zangu mbele yao wakuchao.
26 Maskini watakula na kushiba;wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu watamsifu.Mungu awajalie kuishi milele!
27 Ulimwengu wote utakumbuka na kumrudia Mwenyezi-Mungu;jamaa zote za mataifa zitamwabudu.
28 Maana Mwenyezi-Mungu ni mfalme;yeye anayatawala mataifa.
29 Wenye kiburi wote duniani watasujudu mbele yake;wote ambao hufa watainama mbele yake,wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao.
30 Vizazi vijavyo vitamtumikia;watu watavisimulia habari za Mwenyezi-Mungu,
31 watatangaza matendo yake ya wokovu.Watu wasiozaliwa bado wataambiwa:“Mwenyezi-Mungu ndiye aliyefanya hayo!”