1 Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa,wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange.
2 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,nilikulilia msaada, nawe ukaniponya.
3 Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu;umenipa tena uhai,umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu.
4 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake;kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru.
5 Hasira yake hudumu kitambo kidogo,wema wake hudumu milele.Kilio chaweza kuwapo hata usiku,lakini asubuhi huja furaha.
6 Mimi nilipofanikiwa, nilisema:“Kamwe sitashindwa!”
7 Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu,umeniimarisha kama mlima mkubwa.Lakini ukajificha mbali nami,nami nikafadhaika.
8 Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu;naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu:
9 “Je, utapata faida gani nikifana kushuka hadi kwa wafu?Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu?Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako?
10 Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie;ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!”
11 Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha;umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha.
12 Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya.Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele.