1 Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote,sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake.
2 Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu,wanyonge wasikie na kufurahi.
3 Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami,sote pamoja tulisifu jina lake.
4 Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu,na kuniondoa katika hofu zangu zote.
5 Mgeukieni Mungu mpate kufurahi;nanyi hamtaaibishwa kamwe.
6 Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia,na kumwokoa katika taabu zake zote.
7 Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao,na kuwaokoa katika hatari.
8 Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema.Heri mtu anayekimbilia usalama kwake.
9 Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake;maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu.
10 Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa;lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.
11 Njoni enyi vijana mkanisikilize,nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu.
12 Je, watamani kufurahia maisha,kuishi maisha marefu na kufurahia mema?
13 Basi, acha kusema mabaya,na kuepa kusema uongo.
14 Jiepushe na uovu, utende mema;utafute amani na kuizingatia.
15 Mwenyezi-Mungu huwaangalia waadilifu,na kusikiliza malalamiko yao;
16 lakini huwapinga watu watendao maovu,awafutilie mbali kutoka duniani.
17 Waadilifu wakimlilia Mwenyezi-Mungu yeye huwasikia,na kuwaokoa katika taabu zao zote.
18 Mwenyezi-Mungu yu karibu na waliokufa moyo;huwaokoa wote waliokata tamaa kabisa.
19 Mateso ya mwadilifu ni mengi,lakini Mwenyezi-Mungu humwokoa kutoka yote.
20 Huvilinda viungo vya mwili wake wote,hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.
21 Ubaya huwaletea waovu kifo;wanaowachukia waadilifu wataadhibiwa.
22 Mwenyezi-Mungu huokoa maisha ya watumishi wake,wote wanaomkimbilia hawataadhibiwa.