1 Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni,semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu.
2 Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu.Mwabuduni katika mahali pake patakatifu.
3 Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji;Mungu mtukufu angurumisha radi,sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari!
4 Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu,sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari.
5 Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi;Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni.
6 Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama,milima ya Sirioni kama mwananyati.
7 Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto.
8 Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa,Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi.
9 Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule,hukwanyua majani ya miti msituni,na hekaluni mwake wote wasema:“Utukufu kwa Mungu!”
10 Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika;Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele.
11 Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu!Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani!