1 Kwako, ee Mwenyezi-Mungu, nakimbilia usalama,usiniache niaibike kamwe;kwa uadilifu wako uniokoe.
2 Unitegee sikio, uniokoe haraka!Uwe kwangu mwamba wa usalama,ngome imara ya kuniokoa.
3 Naam, wewe ni mwamba wangu na ngome yangu;kwa hisani yako uniongoze na kunielekeza.
4 Unitoe katika mtego walionitegea mafichoni;maana wewe ni kimbilio la usalama wangu.
5 Mikononi mwako naiweka roho yangu;umenikomboa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu mwaminifu.
6 Wawachukia wanaoabudu sanamu batili;lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu.
7 Nitashangilia na kufurahia fadhili zako,maana wewe waiona dhiki yangu,wajua na taabu ya nafsi yangu.
8 Wewe hukuniacha nitiwe mikononi mwa maadui zangu;umenisimamisha mahali pa usalama.
9 Unionee huruma, ee Mwenyezi-Mungu, niko taabuni;macho yangu yamechoka kwa huzuni,nimeishiwa nguvu mwilini na rohoni.
10 Maisha yangu yamekwisha kwa majonzi;naam, miaka yangu kwa kulalamika.Nguvu zangu zimeniishia kwa kutaabika;hata mifupa yangu imekauka.
11 Nimekuwa dharau kwa maadui zangu wote;kioja kwa majirani zangu.Rafiki zangu waniona kuwa kitisho;wanionapo njiani hunikimbia.
12 Nimesahaulika kama mtu aliyekufa;nimekuwa kama chungu kilichovunjikavunjika.
13 Nasikia watu wakinongonezana,vitisho kila upande;wanakula njama dhidi yangu,wanafanya mipango ya kuniua.
14 Lakini mimi nakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu.Nasema: “Wewe ni Mungu wangu!”
15 Maisha yangu yamo mikononi mwako;uniokoe na maadui zangu,niokoe na hao wanaonidhulumu.
16 Uniangalie kwa wema mimi mtumishi wako;uniokoe kwa fadhili zako.
17 Usiniache niaibike ee Mwenyezi-Mungu,maana mimi ninakuomba;lakini waache waovu waaibike,waache wapotelee kwa mshangao huko kuzimu.
18 Izibe midomo ya hao watu waongo,watu walio na kiburi na majivuno,ambao huwadharau watu waadilifu.
19 Jinsi gani ulivyo mwingi wema wako,uliowawekea wale wanaokucha!Wanaokimbilia usalama kwakowawapa mema binadamu wote wakiona.
20 Wawaficha mahali salama hapo ulipo,mbali na mipango mibaya ya watu;wawaweka salama katika ulinzi wako,mbali na ubishi wa maadui zao.
21 Asifiwe Mwenyezi-Mungu,maana amenionesha fadhili zake kwa namna ya ajabu,nilipozingirwa kama mji unaoshambuliwa.
22 Nami niliogopa na kudhani kwamba ulikuwa umenitupa;kumbe, ulisikia kilio changu nilipokuita unisaidie.
23 Mpendeni Mwenyezi-Mungu, enyi watakatifu wake wote.Mwenyezi-Mungu huwalinda watu waaminifu;lakini huwaadhibu kabisa wenye kiburi wanavyostahili.
24 Muwe hodari na kupiga moyo konde,enyi nyote mnaomtumainia Mwenyezi-Mungu.